.

Chanzo cha picha, YASUYOSHI CHIBA/AFP/Getty Images

    • Author, Abdalla Seif Dzungu
    • Nafasi, BBC Swahili
    • X,

Ni viongozi wachache wa Afrika ambao wamepitia barabara nyembamba ya kuwa na mamlaka na kufuata kanuni.

Katika miongo mitano ya mazingira ya kisiasa yenye misukosuko nchini Kenya, Raila Odinga amefanya maamuzi ambayo yamewatia moyo mamilioni – na kuwashangaza wengi.

Kuanzia kukubali matokeo ya uchaguzi yenye utata hadi kujiapisha kama ”Rais wa Watu”, njia ya Raila haijawahi kuwa ya moja kwa moja.

Haya hapa maamuzi yake yenye utata ambayo hayakuunda tu urithi wake, bali hatima ya kisiasa ya Kenya.”

Pia unaweza kusoma

1. Muungano wa KANU na LDP

Mwaka 2001, chama cha Raila Odinga cha Liberal Democratic Party (LDP) kiliungana na chama tawala cha KANU chini ya Rais Daniel arap Moi.

Matarajio yalikuwa kwamba wanachama wa LDP, akiwemo Raila, wangezingatiwa kwa uongozi na ushawishi katika mpango wa urithi.

Raila alikuwa amejiweka kwa muda mrefu kama mwanamageuzi.

Hata hivyo, mwaka wa 2002, Moi alimuidhinisha Uhuru Kenyatta, mwanasiasa mpya na mwana wa raiwa wa kwanza wa taifa hilo Jomo Kenyatta, kama mrithi wake – akiwaweka kando Raila na viongozi wengine wakuu wa LDP.

Hatua hiyo ilienda kinyume na maono ya Raila ya demokrasia ya ndani na uwazi.

Walitarajia mchakato wa uteuzi wa kidemokrasia au angalau mashauriano mazito.

Baada ya kuhisi usaliti na kutengwa, Raila na washirika wake wa LDP (Kalonzo Musyoka, Moody Awori, na wengine) waliamua kuondoka.

Chaguo la Moi kwa Uhuru lilionekana kama pendekezo, si kuonyesha uungwaji mkono wa wengi ndani ya KANU au chama kipya kilichounganishwa.

2. Azimio la Kihistoria la “Kibaki Tosha”

Wakati wa mkutano mkubwa wa kisiasa katika bustani ya Uhuru Park jijini Nairobi, mwaka 2002, Raila Odinga alitangaza hadharani “Kibaki Tosha!”, akimaanisha “Kibaki atatuongoza!”

Kwa kauli hii, Raila aliidhinisha Mwai Kibaki kama mgombeaji urais wa Muungano wa NARC ulioshirikisha viongozi kutoka vyama mbalimbali, akikusanya wafuasi wake na viongozi wengine wa upinzani nyuma ya Kibaki.

Tamko hilo lilisaidia kuunganisha vikosi vya upinzani vilivyokuwa vimegawanyika hapo awali.

Baada ya tamko hilo Kibaki aliyepewa tiketi ya mgombea wa NARC aliibuka mshindi kwa zaidi ya 60% ya kura za urais na kuashiria mabadiliko makubwa katika siasa za Kenya—kuelekea demokrasia ya vyama vingi na mwanzo wa mwisho wa utawala mrefu wa KANU.

Ingawa Raila aliwaudhi baadhi ya wanansiasa na tamko hilo , kiongozi huyo aliibuka kama wakala mkuu wa mamlaka na nguvu ya kisiasa.

.

Chanzo cha picha, Raila Odinga/X

3.Uchaguzi wa 2007: ‘Amani ni muhimu zaidi kuliko cheo’

Kukubali kwa Raila Odinga kuwa Waziri Mkuu mwaka 2008 kulikuja baada ya kipindi kigumu zaidi katika historia ya kisiasa ya Kenya, kufuatia uchaguzi wa urais wa 2007 uliokumbwa na utata.

Uamuzi wake uliwaacha wengi vinywa wazi , haswa wafuasi wake wakuu na washirika wa kisiasa ambao waliamini kuwa uchaguzi uliibiwa.

Raila aliyewania urais kwa tiketi ya chama cha ODM alionekana kuwa anaongoza katika matokeo ya awali, lakini baada ya ucheleweshaji mkubwa na dosari, Tume ya Uchaguzi ya Kenya (ECK) ilimtangaza Kibaki kuwa mshindi katika mazingira ya kutiliwa shaka.

Kibaki aliapishwa haraka haraka katika Ikulu – saa chache baada ya matokeo kutangazwa.

Tangazo hilo lilizua ghasia na machafuko yaliyoenea kote nchini.

Zaidi ya watu 1,100 waliuawa na zaidi ya 600,000 kukimbia makazi yao katika mapigano ya kikabila na kisiasa.

Kenya ilikuwa kwenye ukingo wa vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Kofi Annan, Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa, aliongoza juhudi za upatanishi chini ya Jopo la Umoja wa Afrika la Watu Mashuhuri wa Afrika.

Raila na Kibaki walikubaliana katika mkataba wa kugawana madaraka ili kurejesha amani.

Mnamo Februari 2008, makubaliano yalitiwa saini huku Kibaki akisalia kuwa Rais na Odinga akiteuliwa kuwa Waziri Mkuu, nafasi iliyoundwa mahsusi kupitia marekebisho ya katiba.

Wizara ziligawanywa kati ya ODM na chama cha kibaki cha PNU.

Wengi wa washirika na wafuasi wa Raila waliamini kukubali nafasi ya Waziri Mkuu ilikuwa kuhalalisha uchaguzi ulioibiwa.

Walihisi ODM ilipaswa kushinikiza kufanyika kwa uchaguzi mpya au mageuzi makubwa zaidi.

Hata hivyo, Raila aliweka uamuzi wake kama dhabihu ya umoja wa kitaifa, mara nyingi akisema “amani ni muhimu zaidi kuliko cheo.”

.

Chanzo cha picha, Video Extract

4. Hatua ya Raila kukataa kushiriki katika marudio ya Uchaguzi wa 2017

Mnamo Septemba 1, 2017, Mahakama ya Juu Zaidi ya Kenya ilibatilisha ushindi wa Rais Uhuru Kenyatta katika uchaguzi wa Agosti 8.

Mahakama ilisema kuwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ilishindwa kuendesha uchaguzi kwa kuzingatia Katiba na sheria.

Uchaguzi mpya uliamriwa ndani ya siku 60 – uamuzi wa kihistoria, sio tu kwa Kenya bali ulimwenguni kote

Hatahivyo hatua ya Raila Odinga kukataa kushiriki katika uchaguzi wa marudio wa urais mnamo Oktoba 2017 ilikuwa hatua ya mabadiliko makubwa katika historia ya kisiasa ya Kenya.

Raila na NASA (National Super Alliance) walilalamika kuwa IEBC haikutekeleza mabadiliko yoyote ya maana baada ya uamuzi wa mahakama.

Maafisa wakuu waliohusishwa na uchaguzi wa Agosti 2014 – kama vile Mkurugenzi Mtendaji wa IEBC Ezra Chiloba – walisalia ofisini.

NASA ilitaka kufanyika kwa “uchaguzi mpya, wa kuaminika” chini ya IEBC iliyofanyiwa marekebisho, lakini hilo halikushuhghulikiwa hatua iliomfanya Raila kususia.

Uhuru Kenyatta aligombea bila kupingwa

Idadi ya wapiga kura ilipungua kwa kiasi kikubwa hadi 38%, ikilinganishwa na zaidi ya 80% mwezi Agosti huku Uhuru akitangazwa mshindi kwa zaidi ya 98% ya kura.

5. Uamuzi wa Raila kushirikiana na serikali ya Ruto

.

Chanzo cha picha, KBC

Kizazi cha Z (Gen Z) nchini Kenya kilifanya maandamano makubwa nchini Kenya ikiwemo mitaani na katika mitandao ya kijamii katikati ya mwaka wa 2024, kikipinga: Gharama kubwa ya maisha, Ufisadi serikalini, Ukosefu wa ajira kwa vijana, Kutozwa ushuru kupita kiasi na Ukosefu wa uwajibikaji kutoka kwa viongozi waliochaguliwa.

Maandamano hayo yaliongozwa na vijana na mara nyingi hayakuwa ya upendeleo.

Raila Odinga na wanasiasa wengine wakongwe hapo awali walitengwa na vuguvugu la Gen Z, ambalo lilionyesha kufadhaika sana na tabaka zima la kisiasa, bila kujali vyama.

Baada ya wiki za maandamano na kuongezeka kwa mvutano wa kitaifa, Raila Odinga alitangaza kwamba atashirikiana na utawala wa Ruto kutafuta njia ya mabadiliko, mazungumzo na suluhu kwa lalama za vijana.

Hili lilitazamwa na baadhi ya watu kama jaribio la kuziba pengo kati ya vijana na serikali, huku wengine wakiliona kama mabadiliko mapya ya kisiasa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *