Picha za tingatiga zikibomoa sehemu za Ikulu ya White House zimeonekana katika vichwa vya habari kote duniani.

Mkaazi wa sasa wa jumba hilo, Rais wa chama cha Republican Donald Trump, anajenga ukumbi mpya wa densi katika sehemu ya Mashariki ya Ikulu ili kuweza kupokea karibu watu 1,000 kwa hafla kama vile dhifa za kitaifa.

Mradi huu wa ukarabati ni jambo lililo karibu sana na moyo wa rais, na mara nyingi ameuzungumzia kwa fahari kubwa. Hata hivyo, mradi huo umekumbwa na ukosoaji mkubwa — hasa kuhusu jinsi unavyofadhiliwa.

Trump afurahia ukumbi wake “mpya, mkubwa, mzuri”

Trump anasisitiza kwamba — kwa miaka 150 — serikali ya Marekani imekuwa ikikosa nafasi ya kufanyia mapokezi makubwa katika Ikulu ya White House. Ndiyo maana, “Rais Donald J. Trump ameonyesha kujitolea kwake kutatua tatizo hili kwa niaba ya serikali zijazo na wananchi wa Marekani,” kama ilivyoandikwa katika taarifa ya vyombo vya habari vya Ikulu mnamo Julai 2025.

Kwa eneo la takriban mita za mraba 8,360 (futi za mraba 89,986), ukumbi huo mpya wa densi unaojengwa sasa ni mkubwa kidogo kuliko uwanja wa kandanda. Kulingana na Trump, utagharimu “takriban dola milioni 300” (€258 milioni).

“Nina furaha kutangaza kwamba ujenzi umeanza rasmi katika viwanja vya Ikulu ya White House kujenga Ukumbi mpya, mkubwa, na mzuri wa White House,” Trump aliandika katika mtandao wake wa Truth Social.

Marekani Washington D.C. 2025 | Ubomoaji katika upande wa mashariki wa Ikulu ya White House kwa ajili ya ukumbi wa ngoma wa Trump wa dola milioni 250
Mashine nzito zikitumika kuvunja sehemu ya upande wa Mashariki wa Ikulu ya White House kupisha upanuzi wa ukumbi wa ngoma unaopigiwa chapuo na Rais TrumpPicha: Pedro Ugarte/AFP

Mipango ya awali ilikuwa na uwezo wa kupokea wageni 650. Katika chakula cha jioni na wafadhili matajiri wiki iliyopita, Trump alitangaza kuwa kutakuwa na nafasi ya watu 999.

Mapokezi makubwa ya kitaifa na sherehe nyingine zinazohudhuriwa na watu wengi mara nyingi hufanyika kwenye mahema yanayowekwa kwenye uwanja wa kusini mwa makazi ya rais. Kulingana na Ikulu, ukarabati wa Trump utamaliza mpangilio huu “usio mzuri machoni.”

Serikali imefungwa, lakini inajenga kumbi za starehe?

Trump amesisitiza kuwa hata senti moja ya kodi ya wananchi haitatumika kwa ajili ya ukarabati huo. Kauli hiyo huenda inalenga kueleza kwa nini kazi za ujenzi zinaendelea katikati mwa kufungwa kwa shughuli za serikali ya shirikisho, jambo ambalo limeilemaza serikali ya Marekani kwa takriban wiki tatu na kusimamisha matumizi mengi ya umma.

Wakosoaji wanauona ukarabati huu kama tatizo: “Je, ni haki kwa serikali kutekeleza miradi ya kifahari na yenye mwonekano wa anasa wakati raia wa kawaida wa Marekani wanapata shida kifedha na serikali ikiwa imefungwa, ambapo maelfu ya wafanyakazi wa serikali hawapokei mishahara kwa kazi yao ngumu?” aliuliza Davina Hurt, mkurugenzi wa mpango wa maadili ya serikali katika Kituo cha Markkula cha Maadili, katika Chuo Kikuu cha Santa Clara.

Marekani Washington 2025 | Onyesho la Protect Our Care kwenye jengo la Mkutano Mkuu wa Republican, RNC, unatoa wito wa ufadhili wa huduma za afya wakati wa kufungwa kwa serikali.
Kufungwa kwa serikali nchini Marekani kumevuruga huduma za shirikisho kama Medicare na Medicaid, huku wafanyakazi wengi wakiwa likizo bila malipo.Picha: Paul Morigi/Getty Images

Hurt aliiambia DW kwamba anahisi ukarabati huo wa kifahari hauna maadili kabisa — hasa wakati huu wa kufungwa kwa serikali, ambapo watu wengi wanalazimika kupunguza matumizi yao. “Huu si wakati — na huenda hautakuja kuwa wakati — wa kujenga ukumbi mkubwa wa kifahari,” alisema.

Nani analipia ukarabati huu?

Trump anasema atalipia ukumbi huo mpya yeye binafsi — kwa msaada kutoka kwa watu matajiri na kampuni kubwa. Orodha ya wafadhili iliyotolewa na Ikulu siku ya Alhamisi inajumuisha kampuni ya ulinzi ya Lockheed Martin na kampuni kubwa za mtandaoni kama Microsoft, YouTube, Amazon, na Google. Wakosoaji wameonya kuwa mfumo huu wa ufadhili unaweza kusababisha rushwa.

“Kampuni hizi zinazotoa pesa zinafanya hivyo waziwazi ili kujipendekeza kwa serikali na kutangaza chapa zao mbele ya maafisa wa shirikisho,” alisema Richard Painter, profesa wa sheria za kampuni na aliyekuwa mwanasheria mkuu wa maadili katika serikali ya George W. Bush kati ya 2005 na 2007.

Marekani Washington D.C. 2011 | Kazi za ujenzi karibu na upande wa Magharibi wa Ikulu ya White House.
Katika picha hii iliyopigwa Januari 31, 2011, ujenzi unaendelea karibu na upande wa Magharibi (West Wing), kulia, wa Ikulu ya White House, kushoto, mjini Washington.Picha: Charles Dharapak/AP Photo/picture alliance

Misaada kwa upendeleo kutoka serikali ya Trump?

Kuna hofu kwamba kampuni na hata watu binafsi wanaotoa michango kwa mradi huu wa Trump sasa huenda wanatarajia kupata fadhila kutoka kwa rais baadaye.

Painter anaona mfumo huo wa “toa nikupe” kama hatari kubwa — na anasema unafikia kiwango cha rushwa.

“Hizi ni kampuni zinazotaka kitu kutoka kwa serikali, na zinatoa pesa kwanza kupata ufikiaji kwa rais na maafisa wa juu, na pili, zikitumaini kuwa zitanunua kile wanachokitaka,” alisema Painter. “Wengi, kama Lockheed Martin, wanataka mikataba mikubwa kutoka Wizara ya Ulinzi, kwa hivyo bajeti yetu ya ulinzi ambayo sasa imefika trilioni moja … itaendelea kukua zaidi.”

Mabadiliko ya kihistoria katika Ikulu

Ukarabati wa Trump siyo wa kwanza kwa rais wa Marekani kubadilisha muundo wa makazi rasmi ya Washington tangu ujenzi wake kuanza mwaka 1792.

Marekani Washington D.C. 1950 | Ukarabati wa Ikulu ya White House kwa kutumia saruji na nguzo za chuma.
Rais Harry Truman alikarabati sehemu ya ndani ya Ikulu ya White House mwanzoni mwa miaka ya 1950.Picha: Everett Collection/picture alliance

Marekebisho hayo yanaanzia kwenye uwanja wa tenisi ambao Barack Obama aliubadilisha ili kucheza mpira wa kikapu, hadi ukarabati mkubwa uliofanywa na Harry Truman, aliyekaa kwenye jumba hilo mwaka 1945. Wakati huo, jengo hilo lilikuwa katika hali mbaya kutokana na kutelekezwa kwa miaka mingi.

Ukarabati huo ulihusisha karibu sehemu yote ya ndani na ulijumuisha chumba kipya cha chakula cha jioni kwa wageni wa kitaifa, njia ya bao (bowling alley), na balcony mpya. Ukarabati huo ulidumu kuanzia 1948 hadi 1952.

Ukumbi wa densi wa Trump umepangwa kukamilika kabla ya kumalizika kwa muhula wake mnamo Januari 2029.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *