Onyo hilo la Rais Trump lilisikika kwenye mahojiano na Jarida la Times na kuchapishwa jana Alhamisi, huku Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio, akisema kwa ujasiri kwamba makubaliano hayo ya amani huko Gaza yataendelea kutekelezwa.

Trump alisisitiza kwenye mahojiano hayo akisema hilo halitatokea, wakati alipokuwa akijibu swali kuhusu mipango ya Israel ya kuunyakua Ukingo wa Magharibi ulioko kwenye eneo la Palestina, ambao Israel imekuwa ikiukalia kimabavu tangu mwaka 1967. Amesisitiza kwamba hilo halitatokea, kwa sababu tayari ameyaahidi mataifa ya Kiarabu.

Alisema “Israel haitafanya chochote kwenye Ukingo wa Magharibi. Msiwe na shaka kuhusu hili.. Hawawezi kufanya lolote kwenye Ukingo wa Magharibi. Msiwe na wasiwasi. Israel inaendelea vizuri sana. Hawatafanya chochote huko.”

Akatahadharisha ikiwa watafanya hivyo, Marekani itaacha kabisa kuwaunga mkono.

Wapalestina wapinga maazimio ya Israel

Wabunge wa Israel siku ya Jumatano waliidhinisha miswada miwili iliyofungua njia ya kuunyakua Ukingo wa Magharibi, hatua iliyokosolewa na Makamu wa Rais wa Marekani JD Vance aliyekuwa Israel na ambaye hakusita kuyaunga mkono matamshi hayo ya Trump. 

Israel Maale Adumim 2020 | Mtazamo wa makazi ya Israel katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa
Januari 28, 2020: Picha ikionyesha makazi ya Waisrael ya Maale Adumim, ambayo ni makubwa zaidi ya Israel katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwaPicha: Menahem Kahana/AFP/Getty Images

Wapalestina nao wamepinga vikali mpango huo wa kunyakua baadhi ya maeneo ya Ukingo wa Magharibi, wakiutaja kama hatua ya wazi ya uvamizi na ukiukwaji wa sheria za kimataifa.

Miongoni mwao ni Wasel Abu Yusuf, mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Ukombozi wa Wapalestina PLO, aliyesema bila shaka, kwa kile kinachoonekana sasa, Israel ni kama ililazimishwa tu kusimamisha vita vyake vilivyosababisha mauaji ya halaiki, uharibifu na umwagaji damu huku ikikiuka kabisa sheria za kimataifa.

Aliongeza “Vitendo vya Israel vinaonyesha namna inavyopuuza maazimio halali ya kimataifa na sheria za kimataifa, ikiwa ni pamoja na kuyakataa maazimio yaliyopitishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.”

Mjini Tel Aviv, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio amesema hii leo akiwa ziarani nchini Israel kwamba kuna hatua nzuri zilizopigwa kuelekea utekelezwaji wa makubaliano ya amani kwenye Ukanda wa Gaza yaliyosimamiwa na Marekani.

Amesema hayo alipozungumza na waandishi wa habari akiwa pamoja na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, hii ikiwa ni kulingana na taarifa kutoka ofisi ya Netanyahu.

Maeneo ya Wapalestina Gaza City 2025 | Uharibifu baada ya kuondoka kwa vikosi vya Israel
Mahema yanayotumiwa na Wapalestina waliokimbia makazi yao pamoja na majengo yaliyoharibiwa, baada ya vikosi vya Israel kuondoka eneo hiloPicha: Dawoud Abu Alkas/REUTERS

Erdogan aitaka Marekani kuongeza shinikizo kwa Israel

Na taarifa kutoka Ankara, Uturuki zimesema Rais Recep Tayyip Erdogan ameitolea wito Marekani na mataifa mengine kuchukua hatua zaidi za kuishinikiza Israel kuheshimu makubaliano ya amani ya Gaza ikiwa ni pamoja na uwezekano wa kuiwekea vikwazo ama kusitisha kuiuzia silaha.

Kwenye taarifa yake alipokuwa akitokea Oman, Erdogan amelisifu kundi la Hamas akisema limeendelea kuheshimu makubaliano hayo na kwamba Uturuki itaendelea kusaidia kikosi kazi kilichoundwa kwa ajili ya kuisaidia Gaza kwa namna yoyote watakavyohitaji.

Na huko Brussels, Viongozi wa Umoja wa Ulaya wamesema sasa wanaangazia namna watakavyoweza kuwa na nafasi kubwa zaidi huko Gaza na Ukingo wa Magharibi baada ya kutengwa kwenye makubaliano hayo. Kwenye mkutano wa kilele uliofanyika Alhamisi mjini Brussels, viongozi hao waliangazia usitishaji mapigano ambao bado unayumba huko Gaza na kuahidi kusaidia juhudi za kuleta utulivu katika eneo hilo la pwani lililoharibiwa na vita.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *