Marekani. Hakuna ubishi zipo filamu nyingi  zinazohusiana na  simulizi za kidini hususani za Yesu Kristo, lakini filamu iitwayo Jesus ndio iliyobamba zaidi na kutumika kusambaza Injili sehemu mbalimbali duniani.

Filamu hii iliyorekodiwa na kuachiwa mwaka 1979 iliigizwa huko Israel na ilijikita zaidi katika andiko la kitabu kilichopo ndani ya Biblia kiitwacho Injili ya Luka.

Kwa mujibu wa taarifa kuhusu filamu hiyo inaelezwa ina asilimia 90 ya usahihi wa andiko la Injili ya Luka.

YE 01

MUIGIZAJI KINARA
Katika filamu hii iliyotengenezwa na Kampuni ya Warner Bros ikishirikiana na The Genesis Project na ilirekodiwa kwa Lugha ya Kiingereza na imetafsiriwa zaidi ya lugha 2,000 ikiongoza katika historia ya filamu zilizotafsiriwa duniani.

Muigizaji mkuu wa filamu hii ni Brian Deacon, raia wa Uingereza ambaye hakuwa maarufu kabla ya kuigiza filamu hiyo ya Jesus.

Mwamba huyu ambaye amesababisha baadhi ya waumini wa Kikristo kutumia taswira ya sura yake katika majumba yao na hata katika majengo ya Ibada kwa kuamini ni Yesu halisi, alizaliwa Februari 13, 1949 katika jiji la Oxford, England.

Deacon ni mtoto wa pili katika familia ya baba aliyekuwa fundi makenika na mama muuguzi.

Deacon alifunga ndoa ya kwanza na Rula Lenska ilivunjika ambapo alizaa naye binti aitwaye Lara Deacon.

Kisha alifunga ndoa ya pili na mwanamama Mfaransa Natalie Bloch, mwaka 1998 hadi sasa wapo katika ndoa hiyo.

Deacon alianza kuigiza mwaka 1971 akianzia kama mwigizaji wa jukwaani na katika runinga mbali kisha  kucheza filamu kadhaa kabla ya kulamba dili la kuigiza filamu hiyo ya Jesus na hata baada ya hapo aliendelea kuangusha moja moja na kazi yake ya mwisho ni Mistaken ya mwaka 2013.

YE 02

ALIVYOPENYA KUIGIZA
Aliigiza filamu ya Jesus hiyo baada ya kupita katika mchujo mkali wa waigizaji zaidi ya 1,000 waliofanyiwa usaili na mtayarishaji John Heyman, huku 260 wakijaribishwa kuigiza (screen test) kuona kama wanafaa.

Deacon alikuwa ni Mwingereza pekee kati ya waigizaji Waisrael,  walioingia katika usaili huo, huku yeye akiwa chini ya Kampuni ya New Shakespears alikokuwa akifanya sanaa za majukwaani na uigizaji.

Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali vya habari, vimefichua Deacon alipata dili hilo kama zali kutokana mchujo mkali ulioendeshwa na watayarishaji ambao walitaka mwigizaji asiue na umaarufu mkubwa, mwenye uso na tabia ambazo zingewafanya watazamaji wamtazame kama Yesu na sio nyota wa filamu.

Inaelezwa yalifanyika majaribio au mitihani ya muda mrefu na mchizi alipenya kutokana na kuwavutia watayarishaji kwa uso wake wa unyenyekevu, tabia ya utulivu na uwezo wa kuonyesha hisia za huruma na hekima, sifa walizoziona zikilingana na sura ya Yesu katika Biblia.

Inaelezwa baada ya kupenya Deacon aliandaliwa kiroho na kihisia, akijifunza kuhusu desturi za Kiyahudi na maisha ya kipindi cha Yesu kulingana na andiko la Injili ya Luka.

Kumbuka filamu hii ilienda kurekodiwa Israel katika maeneo ya kihistoria yanayofanana sana na yaliyotajwa katika Biblia ikiwamo Bahari ya Galilaya na Yerusalemu na walioshiriki kama watazamaji au wale wafuasi na wanafunzi wa Yesu asilimia kubwa walikuwa ni wakazi wa Israel wakiwamo wasanii wasio maarufu ili kutoa uhalisia wa filamu hiyo.

Deacon aliwahi kunukuliwa kukaa katika mazingira halisi ya Israel na kusoma andiko la Injili ya Luka ili kwenda na skripti ilivyokuwa inataka, ilimsaidia kuingia katika nafsi ya Yesu kihisia.

“Sikujaribu kuwa Yesu  nilijaribu kumwakilisha mtu aliyekuwa na upendo, hekima na maumivu ya binadamu kwa njia ya kweli,” alinukuliwa Deacon akielezea hisia alizokuwa nazo.

YE 03

KABLA YA KUICHEZA
Deacon alifichua kabla ya kuchaguliwa kuigiza filamu hiyo, mtihani wake wa kwanza ulikuwa ni kutoka kwa wakala wake,  aliyemvunja moyo kwa kumchana akimweleza kuwa,  hadhani kama yeye (Deacon) atafaa kumwigiza Yesu, lakini anasema alifanikiwa kwa kuamini kipaji alichokuwa nacho. 

Deacon alifichua aliambiwa na mwongozaji (Peter Sykes) asiigize kwa nguvu, bali aonyeshe utulivu na nguvu za ndani, kwamba ufufuo ni ushindi wa kimungu, si wa kibinadamu.

Anasema alifanikiwa kucheza kwa umahiri na ufanisi mkubwa filamu hiyo.

Hata hivyo, kabla ya kuicheza kambini alikuwa na wakati mgumu kutoka kwa watu ambao kila mmoja alikuwa anajaribu kumweleza jinsi anavyotakiwa kuigiza filamu hiyo na hata kuipozi sauti yake na mambo mengine, japo  yeye aliwajibu kwa upole kwa kuwaambia;  “Nitatumia sauti yangu na maelezo kutoka kwa muongozaji.”

Alifichua kwa kusema wiki tatu kabla hawajaanza kurekodi filamu hiyo, alisoma kitabu cha Injili ya Luka zaidi ya mara 20 ili kushika vyema kile alichoelekezaa kwa vile  filamu hiyo imenukuliwa kutoka kitabu hicho.

BAADA YA FILAMU
Deacon anafichua mara baada ya kuigiza filamu hiyo ya Jesus alipata changamoto nyingi za kisaikolojia na utambulisho, kwani watu wengi walimchukulia kama Yesu wa kweli, kiasi kuna waliokuwa wakimsujudia na kutaka awafanyie miujiza, japo anafurahi jamii nyingi ikibadili fikira na maisha yao kiimani kupitia filamu hiyo.

“Nimefurahi kuwa sehemu ya kazi iliyogusa maisha ya mamilioni ya watu,” alisema Deacon.

Ukweli ni kwamba, mwigizaji huyo hakuwahi kudai, yeye ni Yesu, lakini alipata mshtuko wa kisaikolojia wa kijamii baada ya filamu.

Kwa muda mrefu, watu duniani kote walimwona kama ‘Uso wa Yesu’.
Wengine walimsujudia au kumwomba baraka.
Wapo pia waliodhani kweli yeye ni mtu wa kiroho au mjumbe wa Mungu.

Jambo hilo linaelezwa ilimfanya Deacon aishi maisha ya kujitenga kwa muda, kwani hakuwa tayari kuwa ‘ishara ya kidini’ na  badala ya mwigizaji tu.

Katika mahojiano aliyowahi kuyafanya baadaye, alikiri ilimchukua miaka kadhaa kurudi katika hali ya kawaida ya maisha, kwa sababu kila mahali alipokwenda, watu walimhusisha na taswira ya Yesu.

“Nilikuwa tu mwigizaji, lakini ghafla uso wangu ukawa sehemu ya maombi ya watu. Ni jambo zuri, lakini ni zito sana kubeba,” alinukuliwa Deacon akisisitiza hakusumbuliwa kihisia kwa ‘kudhani yeye ni Yesu,’ bali alilemewa na utambulisho wa Yesu uliowekwa juu yake na jamii hadi sasa duniani.

YE 04

KAZI NYINGINE
Licha ya kwamba  filamu ya Jesus (1979) ndio maarufu zaidi, Brian Deacon aliigiza katika filamu na tamthilia nyingi kabla na baada ya kazi hiyo iliyompa heshima na umaarufu mkubwa.

Baadhi ya kazi nyingine za Deacon ni;
‘Vampyres’ (1974), ikiwa ni filamu ya kisayansi ya kutisha.

‘The Triple Echo’ (1972) aliyoshirikiana na Glenda Jackson, ikisimulia kuhusu mwanamke anayemficha mwanajeshi wakati wa Vita Kuu ya Pili.

Pia aliigiza ‘A Zed & Two Noughts’ (1985), ikiongozwa na Peter Greenaway.

‘The Monster Club’ (1981), filamu ya hadithi za kutisha.
Pia kacheza ‘A.D. (Anno Domini)’ (1985),  tamthilia ya Biblia kuhusu historia ya Kanisa la kwanza (aliigiza kama James, si Yesu). ‘The Feathered Serpent’ ya mwaka 1976-1978 na tamthilia iitwayo Lillie iliyoigizwa mwaka 1978 akitumia jina la Frank Miles.

Pia ameshiriki katika vipindi vya televisheni vya Uingereza kama ‘Doctor Who’,  ‘Touch of Frost’, na ‘The Bill’.

Hivyo, ingawa watu wengi wanamjua Deacon kwa filamu ya Jesus, lakini yeye ni mwigizaji mwenye wigo mpana wa kazi nyingine.

YE 05

NYINGINE ZA YESU
Licha ya Jesus kuwa maarufu zaidi, lakini zipo filamu nyingine kadhaa zilizohusiana na Yesu Kristo kulingana na mafundisho ya Biblia.

Baadhi ya filamu hizo ni;
‘The Greatest Story Ever Told’ (1965) iliyoingizwa na Max von Sydow, raia wa Uingereza mwenye asili ya Sweden iliyorekodiwa Marekani (Arizona & Utah).

‘Jesus of Nazareth’ (1977), ikichezwa na mwigizaji wa Kiingereza, Robert Powell na kuongozwa na Muitaliano Franco Zeffirelli.
Filamu nyingine ni ‘The Passion of the Christ (2004), iliyoigizwa na Mmarekani Jim Caviezel na kuongozwa na Mel Gibson, ikiwa imejaa mateso na ukatili wa kuogofya ikitumia lugha za Kiaramu, Kiebrania na Kilatini  ili kutoa uhalisia wa kihistoria.

Hii ndio inatajwa kama filamu ya Biblia iliyopata mapato makubwa zaidi duniani.

Pia ipo ‘The Last Temptation of Christ’ (1988), iliyoigizwa na Mmarekani Willem Dafoe na kuongozwa na
Martin Scorsese raia pia wa Marekani.

Hii Ilipigwa marufuku katika baadhi ya nchi za Kikristo kwa kuonekana ‘kukosa heshima’ kwani ilikuwa na mtazamo wa 
kisanaa, kifalsafa na si wa kidini kama zilizotangulia hapo juu.

Nyingine ni  ‘Son of God’ (2014), iliyoigizwa na Mreno Diogo Morgado ikitokana na mfululizo wa maudhui ya tamthilia ya kwenye runinga ya The Bible (2013).

Ikielezwa ni moja ya filamu iliyoingiza maelfu ya vijana katika mazungumzo ya imani kutokana na wepesi wake wa kueleweka na jinsi ‘Yesu’ alivyoigizwa kisasa zaidi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *