Tangazo hilo kutoka Ikulu limekuja sambamba na onyo kali kutoka kwa Jeshi la Polisi, likiwataka wananchi kuepuka maandamano au kauli za uchochezi siku ya uchaguzi.
Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, amesema jeshi limejipanga kuhakikisha amani inatawala katika kipindi chote cha uchaguzi, na kwamba yeyote atakayevuruga utulivu atachukuliwa hatua za kisheria.
Amezungumza hayo jijini Dar es Salaam wakati wa kongamano la vijana wa vyuo vikuu lililokuwa na kaulimbiu “Nafasi ya Wanavyuo katika Kukuza Amani Wakati wa Uchaguzi Mkuu.”
“Jeshi la Polisi halitasita kuchukua hatua kali dhidi ya mtu yeyote atakayehatarisha amani au kuvunja sheria siku ya uchaguzi.”
EAC kufuatilia mwenendo wa uchaguzi
Wakati hayo yakijiri, waangalizi wa uchaguzi kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wamewasili nchini kufuatilia mwenendo wa uchaguzi huo wa Oktoba 29.
Ujumbe huo unaundwa kwa mujibu wa agizo la Baraza la EAC linalohitaji chaguzi za nchi wanachama zifuatiliwe kwa karibu.
Kiongozi wa ujumbe huo, ambaye pia ni Makamu wa Rais wa zamani wa Uganda, Dkt. Speciosa Wandera Kazibwe, amesema jukumu lao ni kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani na uwazi.
“Tunakuja kushuhudia na kusaidia kuhakikisha kwamba uchaguzi huu unakuwa wa haki, huru na wenye amani.”
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa EAC, Veronica Nduva, amesema ujumbe huo utatoa taarifa ya awali mara tu baada ya upigaji kura, ikifuatiwa na ripoti kamili ya mwisho.
Wakati huo huo, asasi za kiraia zenye mwelekeo wa kijinsia zimewahimiza wanawake na vijana kujitokeza kwa wingi kupiga kura, zikitaja ushiriki wao kuwa msingi wa demokrasia na mabadiliko ya kweli nchini.