Butiama. Mawakala 27 wa mgombea udiwani wa kata ya Masaba, Wilaya ya Butiama, mkoani Mara, kwa tiketi ya ACT-Wazalendo, wamekumbana na kizuizi cha kisheria kuhusiana na kuapishwa.

Msimamizi Msaidizi wa uchaguzi jimbo la Butiama, Charles Kishamuli amesema mawakala hao wameshindwa kuapishwa baada ya kushindwa kukidhi vigezo ikiwa ni pamoja na kutokuwasilisha barua za utambulisho kutoka kwenye chama chao.

Akizungumza na wanahabari kuhusu mawakala wa Kata ya Masaba, kwamba hawakuapishwa baada ya kushindwa kuwasilisha barua za utambulisho  zilizogongwa  muhuri kutoka katika chama chao.

“Mgombea yeye alipeleka orodha ya wagombea aliyoandika kwenye karatasi bila barua ya utambulisho, akapewa maelekezo nini cha kufanya,” amesema.

Amesema pamoja na barua zenye muhuri wa chama pia walitakiwa kuwasilisha picha zao halisi ama leseni ya udereva au kadi ya mpiga kura, vitu ambavyo havikuwasilishwa.

Kishamuli amesema kuwa baada ya mawakala hao kupewa maelekezo, mgombea wao alimpigia simu na alimpa maelezo hayo. Hata hivyo, mgombea huyo hakuridhika na uamuzi huo na kudai kwamba ameonewa.

Amesema kuwa hakuna hujuma yoyote iliyofanywa kwa maelezo hayo, na kuongeza kuwa kama kungekuwa na hujuma yoyote, mawakala wa chama hicho katika kata nyingine pia wangekuwa wamekumbana na kizuizi kama hicho.

Pia, Kishamuli amesema kuhusu kutoapishwa kwa mawakala wengine wa ACT-Wazalendo wa Kata ya Kyanyari kumetokana na wao kushindwa kufika katika ofisi ya kata kwa ajili ya uapisho.

“Mgombea wa kata ile alikuja akaomba mawakala wake wakaapishiwe kwenye kata nyingine, lakini pia wakawa wamechelewa kwa hiyo nimemwambia kama kutakuwa na maelekezo mengine kutoka Tume nitawajulisha na yeye ameridhika,” amesema.

Akizungumza katika ofisi ya kata hiyo leo, Ijumaa, Oktoba 23, 2025, mgombea udiwani, Lucas Magige, amesema kuwa kitendo cha mawakala wake kutokuapishwa ni njama zinazofanywa dhidi yake, ili kumpa fursa mpinzani wake kushinda, kutokana na ukweli kwamba yeye anakubalika zaidi.

“Mimi ninakubalika zaidi, wananchi wanaelewa sera zangu na hii ndio maana wanatumia mbinu zote kuhakikisha nashindwa niiombe Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi kuingilia kati suala hili,” amesema.

Baadhi ya mawakala wamesema wameshangazwa na madai yaliyotolewa na msimamizi huyo kuwa hawajakidhi vigezo ilihali nyaraka walizowasilisha katika ofisi za kata zilitolewa na msimamizi wa uchaguzi jimbo la Butiama.

“Tuliambiwa tupeleka nyaraka zetu ofisi ya msimamizi wa jimbo na sisi tulifanya hivyo, baadaye tukapewa nyaraka ambazo tulikuja nazo huku kwa ajili ya uapisho lakini msimamzi wa kata akasema tunatakiwa kuja na ‘original’ (halisi) na sio ‘photography (nakala),” amesema Juma Magige.

Amesema kuwa baada ya kutokea hali hiyo, walilazimika kwenda katika ofisi ya msimamizi wa jimbo kufuatilia, lakini pia hawakuweza kupata huduma.

Waliporudi katika ofisi za kata, walikuta kwamba muda wa uapisho tayari umeisha.

Kwa upande wake, wakala Bhoke Nguru amedai hali hiyo ni hujuma zinazofanywa dhidi ya mgombea wake ambaye anaonekana kukubalika zaidi kwa wananchi.

Ameongeza tangu awali kulikuwepo na mazingira yasiyokuwa rafiki kwao, kwani hata taarifa ya uapisho walizipata kupitia kwa watu wengine badala ya mamlaka zinazohusika.

“Tulipata taarifa na tulipopiga simu usiku ndipo tulipoambiwa kuwa  uapisho ni kesho yake sasa hapo kama sio hujuma ni nini,” amedai.

Shughuli ya uapishaji wa mawakala kwenye kata hiyo ilifanyika Oktoba 22, 2025.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *