Dar es Salaam. Tangu Harmonize ameondoka WCB Wasafi zaidi ya miaka mitano iliyopita, kuna nyakati amepitia ambazo kwa sehemu zimechafua, kuonyesha kushuka au kuipa changamoto chapa yake ambayo ameijenga kwa miaka mingi.

Mathalani aliondoka WCB Wasafi akiwa ndiye msanii wa pili wa Bongofleva aliyetazamwa zaidi YouTube nyuma ya Diamond Platnumz, ambaye sasa kwa ujumla anashikilia nafasi ya pili Afrika.

Hata hivyo, ndani ya muda mfupi Harmonize alipitwa na Rayvanny ambaye Oktoba 2023 aliweka rekodi ya kutazamwa mara bilioni 1 YouTube, huku Harmonize akifikia mafanikio hayo Novemba 2023.

Ikumbukwe baada ya miaka minne ya mafanikio katika muziki na kutambulika na wengi kama chapa yenye ushawishi, mwishoni mwa 2019, ndipo Harmonize aliamua kuondoka WCB Wasafi.

Aliondoka akiwa na tuzo mbili, African Muzik Magazine Awards (AFRIMMA) na African Entertainment Awards USA (AEAUSA) 2016, na hadi sasa hizo ndio tuzo pekee kubwa za kimataifa alizoshinda.

Nje ya WCB Wasafi, Harmonize akaanzisha lebo yake, Konde Music Worldwide ambayo ndani ya muda mfupi iliwasaini wasanii sita, kitu kilichoshtua wengi waliohoji ni kwa namna gani ataweza kuwasimamia.

Hofu hiyo ya wengi ikageuka kuwa changamoto ya kweli, na hadi kufikia Mei 2025, wasanii wote ambao ni Ibraah, Country Wizzy, Anjella, Cheed, Killy na Young Skales, wakawa wameachana na lebo hiyo.

Kwa mujibu wa Country Wizzy, mkataba wake na Konde Music ulikuwa wa miaka mitano ila aliachana na lebo hiyo baada ya mwaka mmoja kufuatia kuona waliyokubaliana hayatekelezwi! 

Mbali na hayo, Harmonize amekuwa akikosolewa kwa kushindwa kutengeneza nyimbo kubwa YouTube kama ‘Kwangwaru’, ‘Happy Birthday’ na ‘Bado’ ambao kashirikiana na Diamond.  

Nyimbo hizo ndizo hadi sasa zimetazamwa zaidi (most viewed) YouTube, hivyo katika miaka yake mitano nje ya WCB Wasafi ameshindwa kutoa video ilizofanya vizuri kama hizo au kuzizidi.

Video ya wimbo wake, Kwangwaru (2018) akimshirikisha Diamond pia, ndio iliyofanya vizuri zaidi YouTube upande wa Harmonize ikiwa imetazamwa zaidi ya mara milioni 132.

Baada ya Kwagwaru, video za nyimbo zake zilizofanya vizuri ni Happy Birthday (2017) – milioni 58 na Bado (2016) milioni 41. Hii ni changamoto nyingine inayomkabili nje ya WCB Wasafi na wajibu wake kuwajibu wanaomkosoa.

Vilevile hakuna kipindi maisha binafsi ya Harmonize hasa upande wa mahusiano yalionekana kupitia changamoto kibao kama wakati amekuwa nje ya WCB Wasafi.

Aliondoka WCB Wasafi akiwa na Sarah ambaye alifunga naye ndoa muda mfupi baadaye. Lakini takribani mwaka mmoja mbele, waliachana kisha akawa na Kajala ambaye pia ndani ya muda mfupi waliachana.

Baadaye akawa na mrembo kutokea Australia, Briana ambaye alimtambulisha kwa mashabiki wake Novemba 15, 2021 akiwa Marekani alipokuwa akifanya ziara yake ya kimuzi (tour).

Briana aliwasili Tanzania Novemba 27, 2021, akiwa na Harmonize wakitokea Dubai. Kufika usiku wa Machi 30, 2022, Briana akathibitisha kuachana na Harmonize ikiwa ni takribani miezi mitano ya penzi lao!.

Akaja kurudiana na Kajala lakini mambo yakaenda tena ndivyo sivyo. Harmonize alidai inafikia hatua inaogopa kuingia katika uhusiano maana anaona huwenda mahasimu wake kimuziki wanayatumia vibaya.  

Kwa mujibu wa Harmonize, Sarah alikuwa anatumiwa maneno ya husda na mahasimu wake ili amuache wakiamini yeye ndiye alikuwa anampatia jeuri ya fedha na kuweza kuanzisha miradi mipya.

Changamoto nyingine ni video zake na za wasanii wake kuondolewa YouTube, kitu kilichofanya mashabiki kuamini alikuwa akifanyiwa mchezo mchafu ili kumrudisha nyuma.

Video ya wimbo wa aliyekuwa msanii wa Konde Music, Killy, Ni Wewe (2020) ambao wameshirikiana, iliondolewa YouTube kutokana na malalamiko ya hakimiliki.

Baadaye wimbo wa Harmonize, Sandakalawe (2021), nao uliondolewa YouTube kutokana na masuala ya hakimiliki baada ya kampuni ya usambazaji muziki, Empire kulalamika.

Kabla ya hapo, mnamo Agosti 2020, wimbo wa Harmonize ‘Ameen’ uliondolewa YouTube baada ya msanii mwenzake, Rosa Ree kulalamika ulitumia mdundo wa wimbo wake ‘Kanyor Aleng’ bila idhini yake.

Huo ulikuwa wimbo wake wa pili kuondolewa YouTube kutokana na mdundo wake kusikika kama umenakiliwa. Wa kwanza ni ‘Uno’ ambao mtayarishaji wa Kenya, Magix Enga alidai umenakiliwa kutoka kwake.

Licha ya changamoto hizo, bado Harmonize ameendelea kuwapa mashabiki wake muziki mzuri akiwa tayari ametoa albamu tano ambazo zilikuja baada ya kuondoka WCB Wasafi, akiwa ni msanii wa pili kufanya hivyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *