Marekani. Mtayarishaji wa muziki, Shondrae Crawford maarufu kama Bangladesh, 47, amefunguka alivyokutana na Ludacris, 48, hadi kumtengenezea albamu, Back For The First Time, (2000) ambayo ilimtangaza zaidi rapa huyo.
Ikumbukwe kabla ya kuwa mwigizaji maarufu kwenye mfululizo wa filamu za Fast & Furious, Ludacris alikuwa msanii mwenye kiu ya kutoka kimuziki.
Wakati huo alikuwa akifanya kazi kama mtangazaji wa redio na DJ kwenye kituo cha Hot 97.5 (sasa Hot 107.9) jijini Atlanta nchini Marekani, akitumia jina la Chris Lova Lova.
Bangladesh naye alianza safari yake ya muziki mwishoni mwa miaka ya 1990, huku akiendelea na kazi yake ya saluni. Akiwa hana jina kubwa wakati huo, alianza kutengeneza midundo iliyomfikia Ludacris, ambaye alivutiwa na ubunifu wake.
Na punde tu wakakubaliana kufanya kazi, ndipo Bangladesh akatengeneza albamu ya kwanza yake, Ludacris, Incognegro (1999) iliyofanya vizuri hadi lebo ya Def Jam Records kuamua kumsaini kwa mkataba mnono.
Chini ya Def Jam, Bangladesh akaanda albamu nyingine ya Ludacris, Back For The First Time (2000) aliyompaisha rapa huyo kimataifa ikiwa ni nyimbo kali kama ‘What’s Your Fantasy’ aliomshirikisha Shawnna.
Albamu hiyo iliyoshika nafasi ya nne kwenye chati ya Billboard 200 na kuuzwa zaidi ya nakala milioni tatu, ilimfanya Ludacris kuwa nyota mpya wa Hip Hop duniani.
Katika mahojiano na Jarida la Vibe wiki hii, Bangladesh alisimulia namna alivyokutana na Ludacris na jinsi walivyotengeneza wimbo mkubwa, What’s Your Fantasy (2000).
“Nilianza kufanya kazi na Ludacris kupitia rafiki yetu mmoja. Hii ilikuwa kabla ya sisi wote kuanza rasmi muziki,” alisema Bangladesh na kuongeza.
“Niliponunua mashine yangu ya kutengeneza midundo, nilitengeneza mdundo wa ‘What’s Your Fantasy’ nikiwa nyumbani kwa shangazi yangu. Nilihisi kitu cha ajabu kama ndoto zinaenda kutimia,” alieleza.
Akiendelea kusimulia, Bangladesh alisema Ludacris alikuwa akija kunyoa nywele kwenye saluni yake, ndipo siku moja alimkaribisha ndani ya gari lake kisha kumsikilizisha midundo yake.
“Nilikuwa na midundo minne kwenye kanda. Niliicheza na akaanza kutulia kimya akiangalia dirishani, kama mtu aliyepata kitu alichokuwa akikitafuta. Aliniomba nimpe ile kanda na baada ya siku chache, akanipigia simu akaniambia ‘Njoo sasa hivi, leta kila kitu chako.’ Hapo ndipo safari yetu ya muziki ilipoanzia,” alisema.
Kuanzia hapo, wawili hao wakafanya kazi pamoja hadi kuja na albamu kali zaidi katika historia ya Hip Hop huko Marekani ambayo ilikuwa ngazi ya mafanikio makubwa ya Ludacris.
Haikumpa tu jina Ludacris, bali Bangladesh naye ambaye alikuja kupata nafasi ya kufanya kazi na wasanii wakubwa kama Beyonce, Lil Wayne na Kelis.