César Fierro aliachiliwa huru mnamo 2020 baada ya kukaa gerezani kwa zaidi ya miaka 40. Hadi sasa, hajapokea msamaha wa umma kutoka kwa mamlaka.

Chanzo cha picha, Piano Productions

    • Author, Ronald Alexander Ávila-Claudio
    • Nafasi,

Kuhesabu mchwa, kutazama nzi wakiruka, kukwaruza ukuta kwa kucha, kuimba.

Kwa zaidi ya miaka ishirini, hayo ndiyo yalikuwa maisha ya kila siku ya César Fierro, mtu aliyeishi karibu nusu ya maisha yake katika upweke wa chumba cha gereza.

Mzaliwa wa Ciudad Juárez, jiji la mpakani kaskazini mwa Mexico, Fierro, mwenye umri wa miaka 69, alitumia zaidi ya miongo minne gerezani nchini Marekani, akiwa amehukumiwa kifo katika jimbo la Texas kwa mauaji ambayo hakuyafanya.

Nusu ya muda huo aliutumikia peke yake kabisa, katika hali ya upweke uliomchosha akili na mwili.

“Haki imeninyang’anya kila kitu. Kama yamenikuta mimi, yanaweza kumkuta yeyote. Niko huru, lakini sina muda mrefu wa kuishi,” anasema kwa sauti ya huzuni, akizungumza na BBC News Mundo kutoka chumba kidogo anachoishi juu ya paa la jengo jijini Mexico City.

Mwanzoni mwa miaka ya 1980, Fierro, ambaye wakati huo alikuwa akifanya kazi kama mchuma chili huko El Paso, alilazimishwa na kundi la maafisa wa polisi kutia sahihi hati ya kukiri mauaji ya dereva wa teksi, kulingana na Tume ya Kitaifa ya Haki za Kibinadamu ya Mexico (CNDH).

Pia unaweza kusoma:

Aliachiliwa mwaka 2020. Mwaka huohuo, alianza kushirikiana na mtayarishaji wa filamu Santiago Esteinou kutengeneza “La libertad de Fierro” (2024) filamu ya waraka inayosimulia safari yake ya kuzoea maisha huru baada ya miaka 40 gerezani.

Filamu hiyo, iliyoonyeshwa kwa mara ya kwanza Oktoba 10 mwaka huu kwenye kumbi za sinema za Mexico, na awali katika Tamasha la Filamu la Toronto, ni mwendelezo wa “Los años de Fierro” (2014), pia iliyoongozwa na Esteinou.

Filamu hizo mbili zinatafuta kumrejeshea heshima mtu ambaye haki ilimgeuka kuwa adui.

Licha ya yote, Fierro bado anasubiri kuombwa msamaha rasmi na mamlaka za Ciudad Juárez na El Paso, ambazo hazijawahi kujibu maombi yake.

Kwa sasa, anaendelea kupambana kujikimu, kujenga upya mtandao wa marafiki, na kurejesha afya yake iliyodhoofishwa na miaka ya mateso.

Hii ni hadithi yao.

Kilichomshinikiza kukiri

Mnamo Februari 1979, polisi wa El Paso walipata mwili wa dereva wa teksi, Nicolás Castañón, aliyeuawa kwa risasi karibu na mpaka wa Mexico.

Baada ya miezi mitano, Fierro alikamatwa akiwa amemtembelea kaka yake aliyekuwa gerezani. Alishtakiwa kwa jaribio la kuingiza dawa za kulevya gerezani shtaka alilolikana.

“Walinikagua, hawakupata chochote,” anakumbuka Fierro wakati anazungumza na BBC Mundo.

Cesar Fierro alihukumiwa mwaka 1980 baada ya kulazimishwa kukiri mauaji ya dereva wa teksi.

Chanzo cha picha, Piano Productions

Hata hivyo, akiwa bado kizuizini, alilazimishwa kusaini kukiri mauaji hayo baada ya kupokea simu kutoka Ciudad Juárez.

Polisi walimwambia kwamba Jorge Palacios, afisa wa idara ya siri ya polisi, alikuwa amewakamata mama yake na baba yake wa kambo, na kwamba wangechukuliwa hatua za kikatili iwapo asingekubali kosa hilo.

Miaka kadhaa baadaye, Tume ya Kitaifa ya Haki za Binadamu ya Mexico (CNDH) ilithibitisha simulizi la Fierro.

Katika taarifa yake, tume hiyo ilisema maafisa walimtishia kupitia vitisho vya mateso, jambo lililomlazimisha kukiri kwa hofu.

Mara tu baada ya wazazi wake kuachiliwa, Fierro alikana kukiri huko.

“Nilijitangazia kuwa sina hatia. Nilisaini kwa sababu niliogopa wazazi wangu wangeuawa na polisi wa Juárez,” inasema maelezo mafupi katika Kesi ya Avena, kesi ambayo Mexico iliwasilisha dhidi ya Marekani mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki kwa kukiuka haki za kibalozi za raia wake kadhaa ambao walikuwa wameshtakiwa kwa uhalifu.

CNDH ilibaini pia kuwa Palacios alikuwa mwanachama wa Brigada Blanca, kikundi cha kijeshi kisicho rasmi kilichojulikana kwa vitendo vya mateso nchini Mexico katika miaka ya 1970 na 1980.

Hakukuwa na ushahidi wowote wa kimwili uliomhusisha na mauaji hayo.

Mmiliki wa nyumba aliyokuwa akikodi alithibitisha kwamba Fierro alikuwa nyumbani wakati wa tukio hilo.

Shtaka lote lilitegemea kukiri alilolazimishwa kusaini na ushahidi wa mvulana wa miaka 16 mwenye matatizo ya akili, aliyedai kwamba alimwona Fierro akifyatua risasi ndani ya teksi.

Licha ya udhaifu huo, mwaka 1980 Fierro alihukumiwa kifo kwa njia ya sindano ya sumu.

Mwaka 1994, jaji mmoja alikiri kwamba “kuna uwezekano mkubwa kukiri kwa mshtakiwa kulitokana na shinikizo la polisi wa Ciudad Juárez.”

Lakini kwa sababu ya kanuni za kisheria, hakupatiwa kesi mpya na akaendelea kubaki gerezani.

Fierro ndiye mhusika mkuu wa filamu mbili za hali halisi zilizoongozwa na mtengenezaji wa filamu wa Mexico Santiago Esteinou: "Los años de Fierro" (2014), ambayo inasimulia kesi yake ya kisheria, na "La libertad de Fierro" (2024), ambayo inashughulikia mchakato wake wa kuzoea maisha katika uhuru.

Chanzo cha picha, Piano Productions

Upweke wa gereza

Miaka 45 baadaye, Fierro ni mtu tofauti kabisa na kijana mwenye nywele ndefu na uso wa mraba aliyekamatwa mwaka 1979.

Leo amenyolewa nywele zote kichwani, ndevu za kijivu, na macho yenye historia ya mateso.

Anaogopa treni ya chini ya ardhi ya Mexico City sehemu yenye msongamano mkubwa. Na kwa miaka mingi, ulimwengu wake wote ulikuwa chumba cha mita tatu kwa tatu.

Kwanza alifungwa katika Kituo cha Ellis I, Kaunti ya Walker. Mwaka 1999, alihamishwa kwenda Kituo cha Polunsky, ambako alitumikia kifungo chake kilichosalia katika upweke wa kila siku.

Alikuwa akifungwa saa 23 kwa siku, bila mawasiliano ya kibinadamu wala mwanga wa jua.

Baada ya kujaribu kujiua mara kadhaa, maafisa wa gereza walimnyang’anya choo, mashuka na nguo zake, wakihofia angejidhuru.

Anasema pia alinyanyaswa kimwili na kihisia.

“Walinipulizia gesi, wakinitupia sabuni, wakakataa kunipa chakula. Nilifikiria kujiua,” anakumbuka kwa sauti ya chini.

Hatimaye alijifunza kujidhibiti.

“Nilianza kufanya mazoezi, kuimba, na kuwapuuza. Haijalishi walifanya nini, sikulalamika tena.”

Alinyimwa dawa za kutuliza wasiwasi na msongo wa mawazo, jambo lililomchanganya kwa muda na kumlazimu kufanyiwa tiba ya kisaikolojia baadaye.

Wakati miaka ikisonga, vyombo vya habari vya Marekani vilimtaja kuwa mfungwa aliyekaa muda mrefu zaidi akisubiri kunyongwa nchini humo.

César Fierro anatatizika kujikimu kifedha baada ya kuachiliwa kutoka gerezani. Kwa sasa anaishi katika ghorofa iliyotolewa na Esteinou.

Chanzo cha picha, Piano Productions

Katika kipindi hicho alipoteza mama yake, mtu aliyempenda zaidi na ambaye kila mara aliogopa kusikia kwamba mwanawe alikuwa karibu kuuawa kwa sindano ya sumu.

Mara 17 tofauti, Fierro alipewa tarehe ya kunyongwa. Lakini anasema hakuogopa hata mara moja.

“Mara ya kwanza nilipopangiwa tarehe ya kunyongwa, nilikuwa saa nne tu kabla kufa,” anasema kwa utulivu.

“Sikuwa na hofu. Kwa nini? Kwa sababu sikufanya kosa lolote. Nilijua ukweli utajulikana na kweli ulijulikana.”

Uhuru uliojaa kivuli

Katika mojawapo ya mandhari za mwanzo za filamu La libertad de Fierro (2024), César anaonekana akiwa amevaa barakoa ndani ya gari, akitazama mji mtupu kwa mshangao.

Ni mwaka 2020, kipindi ambacho dunia ilikuwa imesimama kutokana na janga la COVID-19.

Mnamo Mei 14, mahakama ya Texas ilibatilisha hukumu yake ya kifo baada ya kubaini makosa katika kesi.

Alibadilishiwa adhabu kuwa kifungo cha maisha gerezani, lakini akapewa nafasi ya kuachiliwa kwa msamaha wa muda mrefu (parole).

Serikali ya jimbo hilo ilimuachia huru na kumbadilisha kuwa mhamiaji aliyehamishwa kurudi Mexico.

Hata hivyo, hakuwahi kuruhusiwa kukata rufaa dhidi ya hukumu yenyewe, kwani mahakama zilisema aliwasilisha ombi lake kwa kuchelewa.

“Sikuwa na mahali pa kuishi, sikuwa na kazi, sikuwa na marafiki. Sikujua hata namna ya kuishi nikiwa huru,” anasema kwa unyenyekevu.

Maisha gerezani, uhuru gizani

Chanzo cha picha, Piano Productions

“Kwa namna fulani, janga lilinisaidia. Kama maisha yangekuwa ya kawaida, ningeumia zaidi. Lakini kwa sababu kulikuwa na watu wachache mitaani, ilinipa muda wa kuzoea, ingawa bado sijazoea kabisa.”

Mkurugenzi wa filamu, Santiago Esteinou, alimpa Fierro makazi baada ya kutoka gerezani, kwani kipindi hicho kilikuwa kigumu kupata hifadhi kutokana na hali ya afya ya umma. Hadi leo, Fierro bado anaishi katika chumba hicho.

CNDH ilipendekeza serikali ya Mexico imuombe msamaha hadharani, impe msaada wa kisaikolojia, fidia ya kifedha, na kumheshimu kwa kuipa bustani au barabara jina lake lakini hadi sasa hakuna lililotekelezwa.

Anaendelea kupambana kujitegemea na kuzoea maisha ya uraiani.

Amejiunga na masomo ya upishi, akajaribu kufanya kazi mgahawani lakini aliacha kwa sababu ya wasiwasi.

Sasa anafanya mazoezi ya tai chi na anasoma Kiingereza katika kituo cha jamii.

“Wanafunzi wengine wanaona aibu kuzungumza. Wanasema wanaogopa. Lakini mimi siogopi kuzungumza Kiingereza,” anasema kwa tabasamu dogo.

Hata hivyo, bado ana hofu zake.

“Bado ninaogopa. Mbali na treni ya chini ya ardhi, ninaogopa pia mabasi. Mahali penye watu wengi hunifanya nihisi wasiwasi,” anakiri.

“Sijapona kabisa… lakini ninapiga hatua.”

Soma pia:

Imetafsiriwa na Mariam Mjahid

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *