Dar es Salaam. Kitu ambacho hakipingiki ni kuwa kila mmoja wetu iko siku atakufa. Pengine ni kwa sababu ya kutokujua huko tutakakokwenda kuna nini, binadamu kwa kawaida tunaogopa sana kifo. 

Dini nyingi zinatuambia kuwa kifo ni faida kubwa ikiwa maisha yetu hapa duniani yatafuata maagizo ya Mungu, lakini bado uhakika huo hautuondoi uwoga wetu juu ya kifo. 

Vifo vya watu wetu wa karibu huleta machungu makubwa kwani vikishatokea tunajua kuwa hatutawaona tena, lakini Mungu katika wema wake katuwezesha kusahau machungu hayo nasi huendelea na maisha kama kawaida baada ya vifo vya wapenzi wetu. 

Leo napata nguvu ya kuandika kuhusu wenzetu watatu waliofariki  Oktoba, ambao wameacha  kumbukumbu katika tasnia ya muziki wa dansi wa Tanzania. Naandika bila majonzi kwani mambo waliyoyafanya hapa duniani katika uhai wao yameacha kumbukumbu za furaha katika mioyo yetu na hasa kwa kazi zao ambazo bado zinatupa raha miaka mingi baada ya wao kuondoka duniani. 

Nianze kwa kumkumbuka mtangazaji mahiri ambaye aliupenda muziki wa dansi wa Tanzania na kuutangaza kwa lugha ambao iliwafanya wasikilizaji waupende muziki wa dansi wa Tanzania.

Mtangazaji huyu alikuwa pia rafiki mkubwa wa wanamuziki.  Huyu si mwingine bali ni marehemu Julius Nyaisanga. Julius ambaye alifahamika zaidi kwa jina la Uncle J, alitokea Kenya na kuja kujiunga na Radio Tanzania Dar es Salaam.

Julius alikuja na aina mpya ya utangazaji ambayo ilimfanya apate nafasi ya pekee katika nyoyo za wasikilizaji wa RTD kwa miaka yote aliyokuwako huko.

Wakati wa uhai wake Julius alisema alitengeneza staili yake ya utangazaji kwa kumuiga mtangazaji maarufu wa KBC, Leonard Mambo Mbotela aliyejulikana sana kwa kipindi chake ‘Je huu ni uungwana?’ Mbotela alikuja na utangazaji uliochangamsha sana kumsikiliza, na huo ndio ulikuja kuigwa na Nyaisanga.

Nyaisanga alikuwa Producer wa mamia ya nyimbo za bendi zilizorekodiwa na bendi mbalimbali katika studio za RTD miaka ya 80. Nilipata bahati ya kufanya nae kazi wakati nilienda kurekodi nikiwa katika bendi tatu tofauti, Orchestra Mambo Bado, Tancut Almasi Orchestra, na  Vijana Jazz Band. Alishauri vizuri na matokeo yake ni nyimbo nyingi zilizopitia mikononi mwake zingali zinapendwa mpaka leo.

Pamoja na utangazaji, na u-producer wa muziki, alikuwa na tabia ya kutembelea bendi zinapopiga na aliweza hata kutembelea bendi nne au tano kwa usiku mmoja. Na hasa kama bendi iko katika ratiba ya kurekodiwa, alipendelea kuifahamu bendi vizuri kabla haijaja studio.

Wakati nikiwa Tancut Almasi Orchestra Julius aliwahi hata kufika Iringa mwaka 1988 kututembelea muda mfupi kabla hatuja rekodi album iliyokuwa na ule wimbo unaoendelea kudumu majukwaani  uitwao Masafa Marefu, wimbo tuliorekodi miaka ya themanini lakini wanamuziki wengi bado wanaurudia mpaka leo.
 
Nyaisanga alipita kwenye bendi kadhaa kututaarifu kuhusu kuanza kwa radio mpya ambayo ingekuwa katika masafa ya FM, na ndipo muda si mrefu radio inayoitwa sasa Radio One ikaingia hewani wakati huo ikiwa pale katika jengo la NASACO, jengo ambalo lilikuja kuungua na baada ya kukarabatiwa  likaitwa Waterfront.

Pia akiwa Radio One Nyaisanga aliendelea kuwa Nyaisanga, japo sera za Radio One hakika zilikuwa tofauti na zile za RTD, lakini pia huko mchango wake katika muziki ulikuwa mkubwa sana. Hatimaye Nyaisanga alihamia Abood Radio Morogoro ambako alikuweko mpaka hatimaye usiku wa kuamkia 20 October 2013, umauti ukamkuta katika hospitali ya Mazimbu Morogoro.

Mwezi huu pia tunatimiza miaka 21 toka kifo cha mwanamuziki mahiri Ndala Kasheba. Kabla ya kuitwa Ndala Kasheba alijulikana kwa jina la Freddy Supreme. Freddy alianza kujifunza gitaa akiwa na umri mdogo wa miaka 12, alipofika umri wa miaka 17 alikuwa tayari mwanamuziki mahiri wa Orchestre Fauvette, akiwa na wanamuziki wenzie kama Baziano Bweti na King Kiki. 

Mwaka 1968, kundi zima la Fauvette likiwa na wanamuziki tisa lilipanda mashua ya walanguzi wa chumvi na kuvuka Ziwa Tanganyika toka Kongo hadi Tanzania kwa kupitia Kigoma.

Kundi hili lilipoingia Tanzania lilikuwa wageni wa Western Jazz Band, lakini baada ya muda mfupi Fauvette ilitingisha anga ya muziki  Tanzania kwa vibao ambavyo wengi huvikumbuka mpaka leo, kama vile Fransisca, Vivi, Nono na Kalemie, Zula, Bigudi, Jacqueline na vingine vingi. 

Kasheba aliweza kuimarisha jina lake zaidi alipoongeza  umaarufu kwa kuanza kutumia  gitaa la nyuzi kumi na mbili, mwenyewe akiliita nyuzi dazani, hasa alipoanza kulipiga kwa mtindo wa Dukuduku akiwa Safari Sound Orchestra. Pamoja na bendi hizo Kasheba pia alipitia  Safari Nkoy, Zaita Muzika, Kasheba group, pia alipita Maquis.

Na kwa wiki chache alipitia Tancut Almasi. Kasheba alifariki 22 Oktoba 2004 akiwa na miaka 58 na alizikwa Kinondoni na gitaa lake. Shabani Yohana Mwanasande, aliyejulikana kwa jina la  Wanted, jina lilopewa na Hemedi Maneti baada ya kumshawishi kuhama Tancut Almasi hakufariki mwezi Oktoba bali alizikwa mwezi Oktoba ikiwa ni zaidi ya mwezi kutoka alipofariki , hii ilitokana na mazingira ya kifo chake. 

Shaban Wanted Yohana, jina lake halisi lilikuwa Cloud Yohana Mwanasande. Alifariki akiwa peke yake chumbani kwake huko Botswana kati ya tarehe 12 na 13 Septemba 2017, na mwili wake kugundulika siku chache baadaye, jambo lililofanya mwili wake kuwa chini ya vyombo vya usalama vya Botswana kwa muda mrefu, ili kupata ukweli kuhusu kifo chake.

Jamii ya Watanzania na wanamuziki wenzake wa huko Botswana kwa kuchangishana na hata kufanya onyesho maalumu la muziki waliweza kupata fedha za kufikisha mwili wa Shaaban mpaka Dar es Salaam. Mwili wa Shabani uliwasili tarehe 9 Oktoba 2017 ukapokelewa na wanamuziki wa Tanzania, na kesho yake  ukasafirishwa na kuzikwa  kwao Michungwani Muheza.

 Shabani Yohana atakumbukwa kwa nyimbo zake alizorekodi kati ya mwaka 1988 hadi 1995 akiwa katika bendi za Tancut Almasi Orchestra, Vijana Jazz Band, na Ngorongoro Heroes. Baadhi ya nyimbo ambazo alipiga gitaa la solo na  bado ni maarufu ni

Nimemkaribisha Nyoka, Masafa Marefu za Tancut Almasi, Azza , Penzi Haligawanyiki, Thereza za Vijana Jazz Band, Kamwembwe  na Naachia Ngazi – Ngorongoro Heroes

Mungu awalaze pema wenzetu hawa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *