d

Kiongozi wa upinzani nchini Cameroon, Issa Tchiroma Bakary, ambaye amejitangaza mshindi wa
uchaguzi uliofanyika tarehe 12 Oktoba, ameiambia BBC kwamba hatakubali kura kuibiwa, huku matokeo rasmi
yakitarajiwa kutangazwa kesho Jumatatu.

Bakary amesema
timu yake imekusanya matokeo kutoka vituo mbalimbali vya kupigia kura na kwamba
“hakuna shaka kabisa” kuhusu ushindi wake. Mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka
76, aliwahi kuwa waziri serikalini kabla ya kujitenga na Rais Paul Biya, mwenye umri wa miaka 92, ambaye
anatafuta muhula mwingine baada ya kuwa madarakani kwa miaka 43.

Chama tawala
kimepinga madai ya ushindi wa Bakary, kikiyaita kuwa ni kinyume cha sheria kwa
sababu ni Baraza la Katiba pekee
ndilo lenye mamlaka ya kutangaza matokeo rasmi.

Katika mahojiano
nyumbani kwake mjini Garoua,
kaskazini mwa Cameroon, Bakary alisema amewahimiza wafuasi wake kulinda kura
zao. “Hatutakubali kura zao kuibiwa na mtu yeyote,” alisema akiwa amevalia joho
jeupe lenye mapambo ya dhahabu.

Waziri huyo wa
zamani alisema hana wasiwasi kuhusu kukamatwa au kufungwa gerezani. “Lakini
najua tayari nimeshinda uchaguzi wa urais,” alisisitiza. “Hakuna shaka, wala
kivuli cha shaka. Ushindi wangu haupingiki.”

Akihoji uwezo
wa Biya, rais mzee zaidi duniani
kwa sasa, kuendelea kushikilia wadhifa huo, Bakary alisema chama tawala CPDM “kimebanwa ukutani” na hakiwezi
kukubali ukweli wa kura. Alitoa changamoto kwao kuthibitisha kama anachosema si
kweli.

Bakary alitetea uamuzi wake wa kujitangaza mshindi,
akisema sheria “haizuii kufanya hivyo.” Awali, alisema ameshinda uchaguzi huo
kwa takribani asilimia 55 ya
kura, akitaja takwimu zilizokusanywa kutoka asilimia 80 ya wapiga kura wote nchini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *