Dar es Salaam. Jeshi la Polisi nchini limetoa hakikisho kwa Watanzania kuwa hali ya usalama imeimarishwa kikamilifu kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Jumatano, Oktoba 29, 2025, ambapo wananchi watatekeleza haki yao ya kikatiba ya kupiga kura kuwachagua Rais, wabunge na madiwani.

Kupitia taarifa iliyotolewa leo Oktoba 26, 2025 na Msemaji wa Jeshi hilo kutoka Makao Makuu ya Polisi Dodoma, David Misime  wananchi na wageni waliopo nchini wamehakikishiwa utulivu wa hali ya usalama na kutakiwa kujitokeza kwa wingi kwenda kupiga kura bila hofu yoyote.

“Hali ya usalama wa nchi ni shwari sana na hakuna tishio lolote la kiusalama linaloweza kufanya shughuli hiyo isifanyike kwa amani,”amesema Misime.

Jeshi hilo limeeleza kuwa limejipanga vyema kuhakikisha kila eneo nchini linabaki salama kabla, wakati na baada ya uchaguzi, likisisitiza kuwa hatua kali zitachukuliwa kwa mujibu wa sheria dhidi ya mtu yeyote atakayejihusisha na uvunjifu wa amani.

“Atakaye thubutu kuvunja sheria asilaumu hatua zitakazochukuliwa dhidi yake, kwani elimu imetolewa vya kutosha na kwa muda mrefu,” limesisitiza Jeshi hilo.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa wananchi wanapaswa kutumia siku hiyo muhimu kwa utulivu, kushiriki katika zoezi la kupiga kura kwa amani, na kuepuka taarifa au vitendo vyovyote vinavyoweza kuchochea vurugu au taharuki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *