Madrid, Hispania. Mshambuliaji chipukizi wa Barcelona, Lamine Yamal, ameongeza chachu ya joto la El Clasico baada ya kutoa kauli iliyowakera wachezaji wa Real Madrid.

Barca itavaana na Madrid leo Jumapili Oktoba 26, mchezo utakaoamua nani akae juu ya kilele cha LaLiga, wakati kikosi cha Hansi Flick kikiwa pointi mbili nyuma ya vinara hao.

Real Madrid walipigwa El Clasico zote nne msimu uliopita jambo ambalo tayari limewapa uchungu wa muda mrefu na sasa kauli ya Yamal imeonekana kuchoma chumvi kwenye kidonda.

Katika mahojiano kwenye Kings League ya Gerard Piqué, Yamal aliulizwa kama timu ya Porcinos inayocheza kwenye ligi hiyo inafanana na Madrid. Bila kusita akajibu:

“Ndiyo, wanaiba… wanalia… wanafanya mambo yale yale.”

Kauli hiyo imefanya kambi ya Los Blancos kuchukizwa vibaya, ambapo gazeti la Marca limeripoti kuwa wachezaji wa Madrid wamechoka na dharau ya mtoto huyo wa miaka 18.

Taarifa zinaeleza kuwa kikosi cha Xabi Alonso tayari kimejadili maneno hayo mazoezini, na kimetoa ahadi ya kimya kimya. “Tutazungumza uwanjani.”

Hii si mara ya kwanza Yamal kuwasha moto. Msimu uliopita, baada ya Barca kugeuza matokeo na kushinda Copa del Rey, Yamal aliwahi kumwambia Araujo hotelini:

“Wakifunga goli moja sawa… hata mawili sawa. Hawawezi kutushika. Tumeonyesha hilo.” Na siku chache baadaye akazidisha moto:

“Mimi nikishinda, hawawezi kusema chochote. Wakishinda wao ndipo wana ruhusa.”

Yamal aliwafunga Madrid mara tatu na kutoa asisti mbili katika El Clasico nne zilizopita na sasa amerudi kutoka majeraha, akionekana kuwa kivutio kikuu cha mchezo huo utakaopigwa leo Jumapili, Oktoba 26, Santiago Bernabeu.

Hata hivyo, vyombo vya habari vya Madrid vimeitaka Barcelona kumuonya chipukizi huyo:

Marca imeandika:

“Kauli za Yamal ni nzito. Barcelona lazima wamwite pembeni. Hawawezi tu kupuuza.”

Wakati El Chiringuito wakisema ni “maneno ya kashfa”, Defensa Central ikaenda mbali ikisema: “Wakati wa kumrudisha Yamal mahali pake umefika.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *