Liverpool, England. Kocha wa Liverpool, Arne Slot, amesema kipigo walichokipata kutoka kwa Brentford ndicho kibaya zaidi tangu aanze kuwaongoza mabingwa hao wa England, na anakiri kuwa bado hajapata dawa ya kukabiliana na timu zinazocheza mipira mirefu.

Liverpool ilizidiwa mbinu na Brentford ambao waliibuka na ushindi wa 3-2 kupitia mabao ya Dango Ouattara, Kevin Schade na Igor Thiago, wakati mabao ya Liverpool yakifungwa na Milos Kerkez na Mohamed Salah. Kichapo hicho kimeifanya Liverpool kupoteza mechi nne mfululizo za Premier League jambo ambalo Slot hajawahi kukumbana nalo.

Akiongea baada ya mechi, Slot hakuwa na kificho:

“Ndiyo, nafikiri hili ndilo pambano baya zaidi kwangu tangu nifike hapa. Tulishuka kiwango. Muda mwingine tunapokuwa nyuma, tunaonesha msuli. Lakini leo tuliteleza kwenye maeneo yote. Tulishindwa kwenye mipira mirefu, na hata kwenye nguvu,” amesema Slot.

Slot amesema timu nyingi zimeanza kuwatandika kwa mipira ya juu, jambo ambalo limeonekana kuwaudhi Liverpool.

“Kuna namna maalum ambayo timu zinatuchezea. Na kwa sasa, hatujapata majibu. Ukiruhusu bao dakika tano za kwanza, unawapa nguvu. Wanafahamu kabisa nini wanafanya.”

Kwa upande mwingine, kocha wa Brentford Keith Andrews alikuwa na furaha isiyo kifani, akisema ushindi huo ni miongoni mwa mafanikio makubwa kwenye maisha yake ya ufundishaji.

“Nilisema kabla ya mechi kuwa tunahitaji ujasiri. Lakini si ujasiri tu, bali nidhamu, kujitoa, na kutokata tamaa. Tumeifunga Liverpool, mabingwa wa ligi. Huu ni ushindi mkubwa sana kwa klabu na kwa safari yetu mpya.” Amesema Keith Andrews.

Katika mechi ijayo ya EPL Majogoo wa Anfield watakuwa na kibarua kingine kwenye Uwanja wa nyumbani dhidi ya Cystal Palace kabla ya kuikaribisha Aston Villa, Novemba Mosi wakati Novemba 4, 2025 itavaana na Real Madrid kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya kisha kukutana na Man City, Novemba 9 kwenye EPL.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *