Chanzo cha picha, Mwananchi
Kufuatia taarifa za baadhi ya watu kwenye mitandao kutangaza kuandamana, Jeshi la Polisi Tanzania limewahakikishia wananchi na wageni walioko nchini kuwa hali ya usalama ni shwari kuelekea siku ya uchaguzi mkuu utakaofanyika Jumatano, Oktoba 29, 2025.
Katika taarifa iliyotolewa leo, Oktoba 26, 2025, na msemaji wa Jeshi la Polisi kutoka makao makuu Dodoma, Jeshi hilo limesema limejipanga kikamilifu kuhakikisha amani na utulivu vinaendelea wakati wa mchakato mzima wa kupiga kura kwa ajili ya kuchagua Rais, Wabunge na Madiwani.
Taarifa ya Jeshi la Polisi iliyotolewa na msemaji wake, Naibu Kamishna wa Polisi DCP David Misime, imeeleza kuwa hakuna tishio lolote la kiusalama nchini na kuwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kutekeleza haki yao ya kikatiba bila hofu yoyote.
“Hali ya usalama ni shwari sana na hakuna tishio lolote la kiusalama linaloweza kufanya shughuli hiyo ya kupiga kura isifanyike kwa amani. Wananchi mnahakikishiwa amani na usalama wa kutosha siku hiyo ya Jumatano, hivyo mjitokeze kwa wingi kama mlivyojiandikisha kwenda kupiga kura bila hofu yoyote,” taarifa hiyo imeeleza.
Jeshi la Polisi pia limeonya kuwa mtu yeyote atakayejihusisha na vitendo vya uvunjifu wa amani au kukaidi sheria kwa nia ya kuharibu uchaguzi atachukuliwa hatua kali za kisheria.
“Atakaye thubutu kuvunja sheria asilaumu, kwa hatua zitachukuliwa dhidi yake kwa mujibu wa sheria za nchi,” taarifa hiyo imesisitiza.
Awali wakati kampeni za uchaguzi zikiendelea, Rais Samia Suluhu Hassan, anayewania muhula wa pili kupitia chama tawala CCM, alilisitiza pia Oktoba 29 itabaki kuwa siku ya kupiga kura tu.
“Ndugu zangu, tarehe 29 mwezi huu tutoke tupige kura. Mimi ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu. Nasisitiza maandamano yatakayokuwepo ni ya watu kwenda vituoni kupiga kura, hakuna mengine,” amesema Rais Samia katika moja ya mikutano yake.
Kauli hii ya Polisi imekuja kufuatia taarifa zinazozunguka mitandaoni kuhusu kundi la watu wanaodaiwa kupanga maandamano siku hiyo ya uchaguzi mkuu, wakitaka Katiba mpya lakini pia kuonyesha kutoridhika kwao na baadhi ya mambo, ikiwemo madai ya kubanwa kwa haki za kiraia, ukosefu wa demokrasia, na hitaji la kuboreshwa kwa mifumo ya uchaguzi.
Jeshi hilo limeeleza kuwa linafuatilia kwa karibu taarifa hizo, likisisitiza kuwa halitaruhusu mikusanyiko isiyo halali wala vitendo vinavyoweza kuhatarisha usalama wa wananchi na mchakato wa uchaguzi.