TIMU ya Kilimanjaro FF inayomilikiwa na kuendeshwa na Watanzania waishio nchini Sweden, imeshika nafasi ya tatu katika Ligi ya Daraja la Sita kwenye Jiji la Stockholm katika msimu wa 2024-2025 iliyohitimishwa mwezi Oktoba 2025.

Akimtaarifu Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Mobhare Matinyi, wakati wa hafla fupi nyumbani kwa balozi ya kulikabidhi kombe la ushindi wa Bonanza la Serengeti, Mwenyekiti wa Kilimanjaro, Norman Jasson, amesema mwakani wamepania kushika nafasi ya kwanza au ya pili ili waingie Ligi Daraja la Tano. 

Kwa upande wake Balozi Matinyi amewapongeza wachezaji hao na kueleza kwamba ubalozi unaitafutia wadhamini kutoka Tanzania ili mbali ya kucheza soka, timu hiyo pia ilitangaze vema jina la Tanzania na fursa zilizopo nchini katika uwekezaji, biashara na utalii.

Vilevile, Balozi Matinyi amewaambia wachezaji na uongozi wa Kilimanjaro kwamba mipango inaendelea kwa kushirikiana na mamlaka za michezo nchini ili ikifanikiwa basi wachezaji vijana wa Tanzania waende nchini Sweden kuiongezea nguvu Kilimanjaro na pia kuwapa uzoefu wa kucheza Ulaya na pengine kubakia katika timu za Ulaya.

KILI 01

Kwa mwaka huu, timu za Stocksunds IF na IFK Lidingö BK ndizo zimeshika nafasi za juu na hivyo kupanda daraja. Mfumo wa michuano ya soka nchini Sweden una madaraja saba kuanzia ngazi za miji.

Katika hafla hiyo iliyofanyika kabla ya tukio la kuangalia mechi ya Yanga na Silver Strikers kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, nahodha wa Kilimanjaro, Richard Ntirugererwa, maarufu Messy, alimkabidhi Balozi Kombe la Bonanza la Serengeti ambalo ililitwaa mwezi Agosti 2025 nchini Ubelgiji kwa mara ya nne mfululizo.

Timu ya Kilimanjaro leo Jumapili Oktoba 26, 2025, inaendelea na raundi ya pili ya michuano ya mtoano ya Kombe la Stockholm ambapo mshindi wake atashiriki kwenye michuano ya Chama cha Soka cha Sweden (SFF).

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *