LICHA ya kushindwa kutetea taji la ubingwa wa gofu wa Afrika ya Mashariki na Kati baada ya kumaliza katika nafasi ya tatu, timu ya taifa ya wanawake ya Tanzania imemuibua nyota mpya chipukizi, Shufaa Twalib, ambaye uwezo wake mkubwa unamfanya awe hazina mpya ya gofu ya wanawake nchini.
Pamoja na chipukizi huyo kuibuliwa, Mtanzania Neema Olomi ameweza kutenegeneza alama bora kabisa kwa wachezaji binafsi akimaliza na wastani +4 alama ambazo ni pungufu kidogo ya alama za wachezaji wa kulipwa.
Kwa Olomi haikuwashangaza wadau wa gofu kwa sababu amekuwa akifanya vizuri sana katika viwanja vya gofu vya nchini, mshangao ulikuwa kwa Shufaa ambaye mashindano haya yamemtangaza yeye kama nyota iliyoanza kuwaka.
Kuwika kwake kumeongeza nyota mwingine wa gofu katika orodha ya wakali wa gofu ya wanawake ambayo kwa zaidi ya miaka 20 sasa imetawaliwa na majina kama Madina Iddi, Angel Eaton na Hawa Wanyeche.
Ni Neema Olomi tu ndiye mzoefu aliyeshiriki na timu katika michuano ya mwaka huu iliyochezwa kwenye viwanja vya Great Rift Valley Lodgem mjini Naivasha nchini Kenya, mashindano ambayo kwa mara ya kwanza Tanzania haikumchezesha Madina Idd.
Shufaa, ambaye ndiyo kwanza amepandishwa kutoka katika timu ya vijana wa umri chini ya miaka 18, alirudisha jumla ya mikwaju 242 ambayo yalikuwa ni matokea ya 9 kwa ubora katika mashindano ya mwaka huu.
Ingawa alianza vibaya kwa kupiga mikwaju 85 siku ya kwanza ya mashindano, aliweza kurudisha mikwaju 79 siku ya pili na kuyaboresha matokeo yake kwa mikwaju 78 siku ya mwisho ya mashindano na kisha akamaliza na alama +29 katika michuano hiyo.
“Naamini nitafanya vizuri zaidi kama nitaendelea kupata fursa za kushiriki mashindano ya viwango vya kimataifa,” amesema Shufaa kutoka klabu ya Lugalo.
Alama alizopata Shufaa na Olomi ndizo zilizosaidia sana Tanzania kupata nafasi ya tatu nyuma ya Reunion na Kenya ambao ndiyo mabingwa wapya.
Kwa upande mningine, Neema Olomi ndiye alikuwa na matokeo bora kwa Tanzania baada ya kupiga jumla ya mikwaju 220 ambayo yalimfanya awe mshindi wa pili kwa wachezaji binafsi akimaliza nyuma ya Melliyal Schmit wa Reunion.
Alianza na mikwaju 72 siku ya kwanza na baadaye kurudisha mikwaju 76 kabla ya kumaliza mashimo 18 ya mwisho na mikwaju 72 ambayo yalimpa jumla ya mikwaju 220.
“Kama na wenzangu wangepata matakeo mazuri zaidi naamini Tanzania tungeweza kutetea taji letu,” amesema Neema kutoka klabu ya Arusha Gymkhana.
Tanzania imemaliza katika nafasi ya tatu juu ya Uganda, Zambia, Rwanda na Madagascar ambayo ilishika mkia.