LICHA ya Flambeau du Centre ya Burundi kuondoshwa na Singida Black Stars katika raundi ya pili ya mtoano wa Kombe la Shirikisho Afrika, kocha wa kikosi hicho, Rukundo Jean de Dieu, amesema kuna mambo mengi wamejifunza na wanaenda kuyafanyia kazi.
Rukundo amezungumza hayo baada ya timu hiyo kuchapwa mabao 3-1, katika mechi ya marudiano iliyopigwa juzi kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi jijini Dar es Salaam, hivyo Singida kuandisha rekodi mpya binafsi ya kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika kwa mara ya kwanza. Katika mechi ya kwanza iliyopigwa Burundi Oktoba 19, 2025, zilitoka sare ya bao 1-1 na hivyo kufuzu kwa kwa jumla ya mabao 4-2.
Akizungumza baada ya mechi hiyo, Rukundo amesema licha ya kupoteza, wao kama benchi la ufundi na wachezaji kiujumla kuna vingi wamejifunza, hususani kujipanga kukabiliana na timu zenye nyota bora unaposhiriki michuano mikubwa ya Afrika.
“Kiukweli presha ilikuwa ni kubwa kwa sababu tulishindwa kutumia uwanja wetu vizuri, kama unavyojua michuano ya Afrika ikiwa utafeli nyumbani sio rahisi kushinda ugenini, wenzetu walikuwa bora na ugeni wetu umetuangusha,” amesema Rukundo.
Katika mechi hiyo, Flambeau ilitangulia kupata bao la David Irishura, huku ya Singida yakifungwa na Malanga Horso Mwaku, Clatous Chama kwa penalti na Idriss Diomande na kuifanya kuifikia rekodi ya Namungo ambayo ilishiriki kwa mara ya kwanza michuano hiyo msimu wa 2020/21 na kufuzu hatua ya makundi.
Katika makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, Singida imeungana na Azam iliyofuzu kwa kuifunga KMKM mabao 9-0.
Singida ilianza hatua ya kwanza ya michuano hii kwa kuitoa Rayon Sports kutoka Rwanda kwa jumla ya mabao 3-1, huku kwa upande wa Flambeau iliyoaga katika Kombe la Shirikisho Barani Afrika ikiitoa Al Akhdar ya Libya kwa jumla ya mabao 4-3.