Babati. Watu wawili akiwemo mwalimu wanashikiliwa na polisi wakidaiwa kuhamasisha watu wasishiriki uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba 29 mwaka 2025.
Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Manyara, Ahmed Makarani watu hao wamekamatwa kwa nyakati tofauti.
Kamanda Makarani ametaja majina ya watuhumiwa hao kuwa ni Juma Almas mkazi wa kijiji cha Matufa kata ya Magugu na Shekhe Adinani mkazi wa kijiji cha Riroda.
Ameeleza kwamba Adinani ni mwalimu anayefundisha Shule za Riroda Islamic na Shule ya Sekondari Chief Dodo iliyopo kwenye kata ya Riroda.
Kamanda wa polisi wa mkoa wa Manyara kamishna msaidizi mwandamizi (SACP) Ahmed Makarani
“Wanashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kuhamasisha watu kutoshiriki uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba 29 mwaka huu,” amesema Makarani.
Ameeleza kwamba polisi mkoani humo, inatoa rai kwa jamii na wananchi kwa ujumla kuwaripoti watu au vikundi vya watu vinavyohamasisha watu kutoshiriki uchaguzi.
“Pia tunatoa wito kwa wananchi na jamii kwa ujumla kuacha kuhamasisha vurugu na fujo kwa kipindi hiki na badala yake wajitokeze Oktoba 29 kupiga kura kwa amani,” amesema.
Robert Salao mkazi wa Babati ameeleza kwamba suala la uchaguzi ni jambo la kikatiba hivyo linapaswa kufanyika, hivyo tabia ya baadhi ya watu kujitokeza na kuzungumza uchochezi wa kutaka lisifanyike ni makosa makubwa hivyo wachukuliwe hatua.
Mkuu wa Wilaya ya Babati, Emmanuela Kaganda, hivi karibuni akizungumza na waandishi wa habari aliwatoa hofu wananchi kuwa washiriki kupiga kura bila kuwa na hofu wala wasiwasi wowote ule.