
Shirika la umoja wa Mataifa linalohudumia wakimbizi, linasema wimbi la wakimbizi wanaokimbia kutoka Burkina Faso na kuingia Mali, linaongeza hali ya dharura ya kibinadamu, UNHCR sasa ikitaka misaada zaidi kutolewa kuwasaidia.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Tangazo la UNHCR hata hivyo limekuja kipindi ambacho mashirika mengi ya misaada kwenye eneo la Sahel yanakabiliwa na ukata wa fedha kutokana na kupungua kwa ufadhili.
Nchi za Burkina Faso na Mali ambazo zote zinatawaliwa na wanajeshi, zinakabiliwa na mashambulizi ya mara kwa mara kutoka kwa makundi ya kijihadi yanayohusishwa na mtandao wa kigaidi duniani wa Al-Qaeda na Islamic State.
Kwenye taarufa yake, UNHCR imesema raia wanaokimbia kutoka Burkina Faso, wengi ni wanawake na watoto kutoka katika vijiji kadhaa vinavyopakana na Mali na wamekuwa wakikimbia tangu Agosti 5.
Kati ya Agosti 7 na 15 mwaka huu, idadi ya watu waliosajiliwa na Tume ya Kitaifa ya Wakimbizi ya Mali (CNCR) iliongezeka kutoka watu 1,733 hadi 12,000, ikiwa ni sawa na wakimbizi 1,500 kwa siku.
UNHCR sasa inasema Bila usaidizi wa haraka kutoka kwa washirika wa kiufundi na kifedha, maelfu ya wanawake, watoto watakuwa hatarini kutumbukia katika dhiki.