
Rais wa Marekani Donald Trump anataka kuigeuza Venezuela kuwa “koloni” la Marekani, Mwanasheria Mkuu wa Venezuela ameiambia BBC.
Tarek William Saab alisema siku ya Jumapili kwamba wito wa mabadiliko ya
utawala nchini Venezuela ni mbinu ya kutaka kunyakua maliasili za nchi yake,
ikiwa ni pamoja na akiba ya dhahabu, mafuta na shaba.
Mshirika huyo wa karibu wa Rais wa Venezuela Nicolás Maduro, Saab anasema “hakuna shaka” Marekani inajaribu kuipindua serikali ya Venezuela,
akiongeza kuwa ni jaribio la hivi punde katika msururu mrefu wa majaribio kama
hayo “yaliyofeli”.
Marekani ni miongoni mwa mataifa ambayo hayamtambui Maduro kama kiongozi
halali wa Venezuela, baada ya uchaguzi uliopita wa 2024 kukosolewa na wengi
kuwa haukuwa huru na wa haki.
Trump pia amerudia mara kwa mara uwezekano wa kile alichokiita “operesheni
za ardhini” nchini Venezuela, na alisema wiki iliyopita kwamba Marekani “inaangalia uwezekano wa operesehani za ardhini” baada ya kupata udhibiti
wa eneo la bahari.”
Takriban watu 43 wameuawa katika mashamulizi dhidi ya boti zinazodaiwa
kuwa za dawa za kulevya katika pwani ya Amerika Kusini, baada ya utawala wa
Trump kuanzisha mashambulizi mapema Septemba kama sehemu ya vita vinavyodaiwa
kuwalenga walanguzi wa dawa za kulevya.
Wabunge wa Congress nchini Marekani kutoka pande zote mbili za vyama vya siasa, wameibua wasiwasi juu ya uhalali wa mashambulizi hayo na mamlaka ya
rais kutoa amri yafanyike.
Seneta wa chama cha Republican Lindsey Graham aliwaambia waandishi wa
habari Jumapili kwamba mashambulizi ya ardhini ni jambo linaloweza kutokea”,
na Trump alimwambia kuwa anapanga kuwafahamisha wabunge wa Congress
kuhusu operesheni za baadaye za kijeshi atakaporejea kutoka Asia.
Alipoulizwa kuhusu uwezekano wa kuvamiwa kwa ardhi ya Venezuela, Saab ameiambia
BBC “haipaswi kutokea, lakini tumejitayarisha.”
Aliongeza kuwa Venezuela “bado iko tayari kuanza tena
mazungumzo” na Marekani, licha ya mashambulizi “haramu” dhidi ya
ulanguzi wa dawa za kulevya.
Katika kipindi cha miezi miwili iliyopita, Marekani imekuwa ikiendelea
kujenga kikosi cha meli za kivita, ndege za kivita, wanajeshi wa majini, ndege
za kijasusi, na ndege zisizo na rubani katika visiwa vya Caribbean, kama sehemu
ya kukabiliana na ulanguzi wa dawa za kulevya na “magaidi wa
mihadarati.”