Vijana na matumizi ya mitandao

Chanzo cha picha, Getty Images

Binti yake wa miaka kumi na minne alipoanza kuzungumza na vijana wengine kwenye mtandao, mama yake hakuwa na wasiwasi sana.

Lakini wiki chache tu baadaye, Christina (sio jina lake halisi) aligundua kuwa tabia ya binti yake ilikuwa ikizidi kubadilika.

Kijana huyo aliangukia katika kundi la 764, kundi la mrengo wa kulia lenye muelekeo wa Kishetani linalofanya kazi mtandaoni.

Makundi haya yanaundwa zaidi na wavulana vijana na wanaume vijana wanaotaka kuwanyanyasa wasichana.

Unaweza kusoma

Takribani vijana wanne wa Uingereza wamekamatwa kuhusiana na shughuli za kimataifa za kundi hilo, akiwemo mwanachama 764 Cameron Finnegan, ambaye aliishi Horsham, East Sussex, Uingereza. Alihukumiwa kifungo cha miaka sita jela mwezi Januari.

Christina anasema anaamini binti yake alilengwa na Kundi 764 baada ya kushiriki katika chumba cha gumzo mtandaoni kuhusu kujidhuru.

Kundi hilo linawalazimisha waathiriwa kufanya vitendo vya ngono vya waziwazi, kujidhuru, na hata kujaribu kujiua wakati simu za video zikionesha vitendo hivyo mubashara mbele ya wanachama wengine wa kundi.

Christina anasema mwanachama wa Kundi 764 kwanza alipata uaminifu wa binti yake na kisha akamdanganya kufanya vitendo hivi.

“Nilimtazama mama yangu akipigania maisha yake kutokana na saratani ya matiti iliyoendelea, lakini haikuwa vigumu kama kumtazama binti yangu akifa,” anasema.

“Hali yake ilizidi kuwa mbaya zaidi ya ile inayoonekana kwa wagonjwa wa saratani.”

Wafuasi wa kikundi cha 764 wanashiriki picha na video za kutisha

Christina anasema kumwokoa binti yake kutoka kwenye kundi 764 kumekuwa changamoto ngumu kwake.

“Niliendelea kumwambia awazuie, aache kuzungumza nao, lakini sikuweza kufikiria athari waliyo nayo kwa binti yangu na jinsi alivyowaogopa.”

“Walikuwa wamemshawishi kabisa kwamba hakuwa na thamani, wakiwa nao au bila wao.”

Christina na binti yake walijenga upya maisha yao polepole, na anasema anataka wazazi wafahamu hatari za vikundi hivyo.

“Binti yangu halali tena wala hali,” anasema.

“Kama mama, nilihisi nisingeweza. Nilikuwa na hofu, siwezi, na nikakata tamaa.”

Shirika la Kitaifa la Uhalifu la Uingereza linaona vikundi kama 764 kuwa miongoni mwa vitisho hatari zaidi kwenye mtandao.

“Wafuasi wa vikundi hivi wanazidi kuwa vijana na matendo yao hayaripotiwi,” anasema Rob Richardson, naibu mkurugenzi wa kitengo cha kupambana na unyanyasaji na vitisho kwa watoto mtandaoni cha Shirika la Kitaifa la Uhalifu.

Alisema kwamba kutoka kwa mtazamo wa vyombo vya kutekeleza sheria, kuwasiliana na waathiriwa mara nyingi huambatana na matatizo makubwa.

“Mara nyingi waathiriwa hawajioni kama waathiriwa, jambo linalofanya iwe vigumu. Wasichana wako katika hatari zaidi katika suala hili.”

Wazazi wanashauriwa kuzingatia shughuli za watoto wao mtandaoni, kutumia zana za ufuatiliaji wa wazazi, na ikiwezekana, kuwa na mazungumzo yasiyo ya kuwahukumu.

Wakfu wa Molly Rose, ulioanzishwa kwa kumbukumbu ya Molly Russell mwenye umri wa miaka 14, ambaye alijiua baada ya kuhusishwa na maudhui hatari ya mtandao, unaonya kuhusu ukuaji wa haraka na kuongezeka kwa vikundi kama 764.

“Tunajua vinafanya kazi waziwazi mbele ya kila mtu na kwenye mitandao ambayo watoto na vijana wengi hutumia kila siku,” anasema Andy Burrows, mkurugenzi wa wakfu huo.

“Vikundi hivi viko mstari wa mbele kwa kujiua kwa vijana na kujidhuru.”

Mtandao wa 764 uliundwa na kijana wa Marekani anayeitwa Bradley Cuddinhead mnamo 2020 alipokuwa na umri wa miaka 15 tu. Aliita kikundi hicho jina la sehemu ya msimbo wa posta wa mji wake wa Texas.

Polisi wanasema kundi hilo ni sehemu ya mtandao wa kimataifa wa makundi ya mrengo wa kulia na linaendeleza “itikadi kali na za kivita.”

Katika mazungumzo ya mtandaoni, Finnegan, ambaye alijiunga na kundi la 764 baada ya kumnasa binti wa Christina, anajisifu kwa watumiaji wengine kuhusu vitendo vyake vya kuwafanya watoto kujidhuru.

Cameron Finnegan, mfuasi wa Kundi la 764 na mkazi wa Horsham, Uingereza, alihukumiwa kifungo cha miaka sita jela mwezi Januari.

Chanzo cha picha, South East England Counter Terrorism Police

Baada ya kukamatwa kwake, polisi walimuuliza Finnegan, ambaye alikuwa na umri wa miaka 18 wakati huo, alichokijua kuhusu Kundi la 764.

“Wanawanyonya watu kulingana na rangi, matatizo ya afya ya akili au ishara yoyote ya udhaifu wa kiakili ili waweze kuwanyonya,” Finnegan alisema.

Kijana huyo alihukumiwa kwa kuchochea watu kujiua, kumiliki hati za kielimu zinazohusiana na vitendo vya kigaidi, na kumiliki picha zisizofaa za mtoto.

Katika kesi yake, jaji alitangaza kwamba Finnegan alikuwa “hatari kubwa , mwenye madhara kwa jamii.”

Polisi wa kupambana na ugaidi wameonya kwamba kundi hilo ni “tishio kubwa” kwa jamii kwa ujumla.

Claire Finlay, mpelelezi katika Kitengo cha Kupambana na Ugaidi cha Kusini Mashariki mwa Uingereza, alisema: “Kesi ya Cameron Finnegan imeimarisha hitaji la kudhibiti vikundi hivyo kwenye mtandao.”

“Sehemu ya juhudi hizi inalenga tu kuwafanya wazazi na walezi wafahamu vitisho na hali ambazo vijana wanaweza kukumbwa nazo.”

Ukuta wa chumba cha kulala cha Finnegan

Chanzo cha picha, South East England Counter Terrorism Police

Mwaka jana, FBI ilitoa onyo lisilo la kawaida kuhusu Kundi la 764, ikisema kundi hilo linatumia vitisho, ulafi na udanganyifu kuwadhibiti waathiriwa, likiwaomba kupiga picha au kufanya vitendo vya kujidhuru, unyanyasaji wa kingono au hata kujiua kwenye kamera.

FBI ilifichua kwamba ilifanya uchunguzi kwa watu 250 wanaohusishwa na Kundi la 764 na mitandao mingine ya mtandaoni.

Kukamatwa pia kumefanywa kuhusiana na unyanyasaji wa watoto, utekaji nyara na mauaji yanayohusiana na kundi la 764 katika takribani nchi nane, ikiwa ni pamoja na Uingereza.

Afisa Mkuu wa Kesi ya Cameron Finnegan amezungumzia wasiwasi wake kuhusu jinsi vijana wanavyoweza kushawishiwa kufanya uhalifu wa kutisha.

“Wengi wa watu hawa mwanzoni walivutiwa na vikundi kama 764 kwa sababu walidhani ilikuwa ya kufurahisha kuwanyanyasa na kuwadanganya watu walio katika mazingira magumu, na katika kundi hili uelekeo huu wote umekuwa mkali zaidi,” anasema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *