Dar es Salaam. Baada ya picha za msanii Lulu Diva kusambaa mitandaoni akiwa amevaa nguo sare na aliyowahi kuonekana ameivaa msanii wa Bongo Movies, Wema Sepetu na mashabiki kuanza kumshambulia kwamba ameiazima, msanii huyo ameweka rekodi sawa kuhusu stori hizo za mitandaoni.
Akizungumza na Mwananchi Lulu, amesema ameshangaa jinsi watu walivyomshambulia vibaya huko mitandaoni kwamba anaazima nguo kwa Wema wakati siyo kweli.
“Mimi siwezi kuvaliana nguo na mtu yeyote yule, kwa nini nifanye hivyo? Nguo ninazovaa nililinunua mwenyewe dukani kwa pesa zangu, naomba waniache jamani, hebu wafuatilie vitu vya maana kutoka kwangu, wanisapoti hata kwenye huu muziki wangu nitawashukuru sana ila sio kufuatilia mambo ya kizushi.
“Kwanza watu watambue Wema ni pacha wangu, asilimia kubwa ya nguo huwa tunanunua wote, au mmoja wetu akiipenda nguo anamchukulia mwenzake kama hiyo hiyo, hivyo sisi hatuvaliani nguo japo ni marafiki tulioshibana kwa muda mrefu,” amesema Lulu.
Wema na Lulu Diva wamekuwa na urafiki wa muda mrefu. Mwanzoni mwa urafiki wao watu walikuwa hawajawaelewa, walikuwa walimuita Lulu Diva ni chawa wa Wema.
Katika urafiki wao huo wamekuwa wanagombana na kupatana na hawajawahi kuweka wazi chanzo cha ugomvi wao wanapokuwa wamegombana na baada ya hapo wanamaliza ugomvi huo kimya kimya.