Shirika la Kitaifa la Vipaji la Iran (INEF) limeandaa hafla maalum ya kuwatunuku wanafunzi 17 wenye vipaji na vijana waliotwaa medali za dhahabu, fedha na shaba katika mashindano ya kimataifa ya Olimpiadi za Sayansi katika nyanja za Akili Mnemba (AI), Astronomia na Fizikia ya Anga, Uchumi, na Sayansi ya Kompyuta.

Akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika Jumamosi, Naibu Mkuu wa INEF, Saeed Khodaygan, alisema kuwa washindi wa medali za Olimpiadi hujiunga moja kwa moja na “njia ya vipaji,” safari inayowakilisha mwanzo wa ustawi wao wa kisayansi na kipimo halisi cha mchango wao kwa jamii.

Amesisitiza kuwa njia hiyo ni heshima na jukumu kwa wakati mmoja, heshima wanayopewa na jamii, na jukumu la kuitumikia jamii hiyo kwa maarifa na huduma.

Aliwaambia washindi: “Medali yako ni fahari kubwa kwa taifa, lakini ni mwanzo tu wa safari.”

“Katika miaka ijayo, litakalokuwa na thamani zaidi kuliko medali yenyewe ni athari yako kwa jamii na huduma yako ya kisayansi kwa taifa. Hiyo ndiyo medali ya kweli inayotolewa na jamii.”

Afisa huyo aliongeza kuwa njia ya vipaji ni ngumu na yenye changamoto, ikiwakilisha hatua ya mpito kutoka kupokea maarifa hadi kutoa huduma za kisayansi na kijamii.

Aidha amebainisha matumaini  kuwa kwa bidii ya wenye vipaji na msaada wa familia zao, na ushirikiano wa taasisi za kisayansi za taifa, wataendeleza safari ya ukuaji wa vipaji kwa uthabiti ili majina yao yaandikwe kwa fahari katika historia ya Iran.

Mwezi Julai, timu ya baiolojia ya Iran ilitwaa medali 3 za dhahabu na 1 ya fedha katika Olimpiadi ya 36 ya Biolojia ya Kimataifa iliyofanyika nchini Ufilipino, na kujiimarisha miongoni mwa timu bora duniani.

Katika mwezi huohuo, timu ya kitaifa ya Iran ya Olimpiadi ya Hisabati iliangaza katika Olimpiadi ya 66 ya Kimataifa ya Hisabati ya mwaka 2025 nchini Australia, ikishinda medali 2 za dhahabu, 3 za fedha, na 1 ya shaba.

Mwezi Agosti, kwa mwaka wa pili mfululizo, timu ya kitaifa ya Iran ya Olimpiadi ya Astronomia na Fizikia ya Anga ilitwaa ushindi wa juu katika Olimpiadi ya 18 ya Kimataifa ya Astronomia na Fizikia ya Anga (IOAA), iliyoshirikisha mataifa 64.

Timu ya Iran ilionesha uwezo wa kipekee katika mashindano ya mwaka huu na kufanikisha ushindi wa nafasi ya kwanza kwa kutwaa medali 5 za dhahabu kwa mtindo wa kishindo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *