BAADA ya Yanga kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, mabosi wa klabu hiyo wamewatunuku mastaa wa kikosi hicho Sh200 milioni kufuatia kazi kubwa waliyoifanya.
Yanga ambayo ilikuwa na kibarua kizito baada ya kupoteza mechi ya kwanza ugenini dhidi ya Silver Strikers ya Malawi kwa bao 1-0, Jumamosi iliyopita ilishinda nyumbani 2-0 na kufuzu kwa jumla ya mabao 2-1.
Sasa baada ya kupoteza ugenini, mabosi walifanya kikao na mastaa hao hukohuko Malawi, lakini wakaona haitoshi wakawatimbia mazoezini waliporudi nchini.
Kikao hicho cha viongozi na wachezaji kilizaa bonasi iliyowapa morali mastaa hao katika mechi ya marudiano iliyochezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Jumamosi iliyopita.
Katika kikao hicho na mabosi, wachezaji waliambiwa endapo watafanikiwa kuitoa Silver Strikers basi watajiokotea Sh200 milioni.
Mbali na fedha hizo, pia ushindi wa mabao 2-0, umeifanya Yanga kuvuna Sh10 milioni kutoka katika hamasa ya Bao la Mama ambapo timu za Tanzania zinazoshinda mechi za CAF msimu huu kuanzia hatua ya awali, kila bao thamani yake ni Sh5 milioni.
Hivyo basi, bonasi ya Sh200 milioni kutoka kwa mabosi na Sh10 ya Bao la Mama, jumla mastaa wa Yanga wamevuna Sh210 milioni kwa kuichapa Silver Strikers tu.