Brendan Rodgers amejiuzulu nafasi ya umeneja wa Celtic huku Mwanahisa Mkuu wa klabu hiyo Dermot Desmond akimuelezea kocha huyo kuwa ameleta mgawanyiko, mpotoshaji na mbinafsi.

Katika usiku wa kushangaza jana Jumatatu, ilitangazwa muda mfupi kabla ya saa 10 jioni kwamba Rodgers amejiuzulu wadhifa wake, huku Martin O’Neill na Shaun Maloney wakichukua wadhifa wa muda.

Hilo lilikuja baada ya Celtic kuchapwa mabao 3-1 ugenini na Hearts Jumapili, matokeo ambayo yameiacha timu hiyo ikiwa nyuma ya vinara hao wa ligi kwa pointi nane katika mbio za ubingwa.

Mwanzo mbaya wa msimu katika mashindano ya ndani na yale ya Ulaya, umesababisha kuongezeka kwa mvutano kati ya Rodgers, bodi ya klabu na mashabiki wenye hasira.

Desmond ambaye ni Mwanahisa Mkuu wa Klabu hiyo amesema kuwa Rodgers alifanya mambo yasiyostahili ndani ya klabu hiyo.

“Maneno na matendo yake tangu wakati huo yamekuwa ya kugawanyisha, kupotosha na kujinufaisha.

“Wamechangia hali ya sumu katika klabu na kuchochea uhasama dhidi ya wanachama wa timu ya utendaji na bodi,” imesema taarifa ya Desmond.

Rodgers, ambaye mkataba wake ulikuwa unamalizika mwishoni mwa msimu huu, amekuwa akikosoa kile alichokiona kuwa kufeli kimkakati katika kuajiri na ukosefu wa uwekezaji katika dirisha la usajili la majira ya kiangazi.

Katika majira ya joto, walitumia Pauni 13.3 milioni (Sh43.7 bilioni)  kusajili kiasi ambacho ni karibu nusu tu ya kile walichopata kutokana na kuuza wachezaji muhimu.

Pia alikashifu kitendo alichoamini kuwa ni cha ‘uoga’ kutoka kwa afisa wa ngazi ya juu wa klabu ilipodaiwa kuwa Celtic walikuwa wakitoa taarifa dhidi yake kwenye vyombo vya habari.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *