Chanzo cha picha, Reuters
Hofu inaongezeka juu ya mauaji ya halaiki katika mji muhimu wa el-Fasher
nchini Sudan baada ya wanamgambo wa Rapid Support Forces (RSF) kuuteka kutoka vikosi
vya serikali.
Katika hotuba yake Jumatatu jioni, mkuu wa jeshi la Sudan Jenerali Abdel
Fattah al-Burhan alisema ameidhinisha kuondoka kwa wanajeshi ili kuzuia “uharibifu na mauaji ya raia.”
Umoja wa Mataifa umesema kuna ripoti za kuaminika za “mauaji ya kiholela,”
wakati Maabara ya Utafiti ya Chuo Kikuu cha Yale, Marekani ikionesha picha za
satelaiti za “marundo ya miili ya watu waliouwawa kwa makundi.”
RSF imekanusha shutuma za kuua raia au kuyalenga makabila ya watu
wasiokuwa Waarabu, licha ya ushahidi uliotolewa na Umoja wa Mataifa na
mashirika ya kutetea haki za binadamu.
Kuanguka kwa El-Fasher katika eneo la Darfur kunaashiria
mabadiliko makubwa katika vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan, ambavyo
vimeua maelfu na kuwafanya karibu watu milioni 12 kuyahama makazi yao tangu
Aprili 2023.
Wapiganaji wa RSF waliuzingira mji wa el-Fasher wenye maelfu ya raia
kwa muda wa miezi 18, na kupelekea mgogoro wa njaa.
Maabara ya Utafiti wa Masuala ya Kibinadamu ya Chuo Kikuu cha Yale imeiambia
BBC, tangu mji huo kutekwa, picha za satelaiti zimeonyesha “marundo ya
miili iliyouawa kwa pamoja, au iliyopigwa risasi na walenga shabaha.”
Na katika chapisho kwenye X, mkurugenzi mtendaji wa maabara hiyo ameelezea
mshtuko wake kwa kuona “madimbwi ya damu” kupitia picha za satelaiti.
Vile vile, timu ya Umoja wa Mataifa ya kutoa misaada ya kibinadamu
nchini Sudan imesema “imeshtushwa” na ripoti za ukatili kama vile “mauaji ya kiholela,” mashambulizi dhidi ya raia kwenye njia za
kutoroka, unyanyasaji wa kingono na uvamizi wa nyumba hadi nyumba.
Kikosi cha Pamoja, muungano wa makundi yenye silaha ya Darfuri yanayoiunga
mkono jeshi, yamesema raia 2,000 wameuawa tangu mji huo ulipoanguka. Hakuna
uthibitisho wa hili.
Wakaazi waliofanikiwa kutoroka El-Fasher wameiambia BBC, wana hofu baada ya kupoteza mawasiliano na jamaa ambao bado wamekwama jijini.