Chanzo cha picha, Imo State/ Facebook
Jamii iitwayo Awo-Omamma katika eneo la Serikali ya Mtaa ya Oru katika Jimbo la Imo nchini Nigeria imezua gumzo mtandaoni baada ya familia moja kumlazimisha mwanamke kunywa maji yaliyotumika kuosha maiti ya mume wake.
Chika Ndubuisi, alipitia hali hiyo baada ya mumewe kufariki.
Familia ya mumewe ilimkamata, ikamshtaki kwa mauaji, na kumlazimisha kunywa maji yaliyotumika kuosha mwili wa mumewe aliyefariki ili kuthibitisha kutohusika na kifo cha mumewe.
Hilo lilifanya serikali ya Jimbo la Imo kuwasiliana na Wizara ya Masuala ya Wanawake, ambayo ilikimbia hadi eneo la tukio na kumuokoa mwanamke huyo.
Serikali ya Jimbo la Imo ilisema nini
Serikali ya Jimbo la Imo kupitia Kamishna wa Wanawake na Maendeleo ya Jamii, Nkechinyere Ugwu, imelaani tukio hilo baada ya kumuokoa mwanamke huyo (Chika Ndubuisi).
Katika barua waliotoa, walieleza kile ambacho familia hiyo ilimfanyia Chika Ndubuisi kuwa ni kitendo kibaya na cha kusikitisha sana.
“Hili ni jambo baya sana. Ni kinyume cha sheria na haikubaliki katika ulimwengu ulio wazi,” Serikali ya jimbo ilisema.
Je, waliomfanyia Chika Ndubuisi kiendo hicho watafanywa nini?
Kamishna Nkechinyere Ugwu alisema katika barua iliyotolewa na ofisi yake kuwa waliotenda kitendo hicho kwa mjane huyo, hatimaye watajua kuwa kuna sheria inayoongoza nchi.
Alisema kuwa “watu hao watakwenda mahakamani kujibu walichofanya”.
Aidha alisema kuwa serikali ya Jimbo la Imo ina nia ya kulinda haki na utu wa wanawake katika jimbo hilo.
Hali ya sasa ya Chika Ndubuisi
Wizara ya Wanawake na Maendeleo ya Jamii ya Jimbo la Imo imethibitisha kuwa Bi Chika Ndubuisi kwa sasa amelazwa hospitalini.
Ilisema mwanamke huyo pia yuko mahali ambapo atapewa moyo, ushauri na msaada kwa ajili ya afya yake ya akili, yaani ‘psychosocial support’ kwa Kiingereza.
Walisema kama kawaida, polisi wameanza uchunguzi kubaini kilichotokea.
Je, kuna sheria dhidi ya kile kilichotokea kwa mwanamke huyu?
Wakili maarufu katika Jimbo la Enugwu ambaye pia ni gavana wa zamani, Nnenna Anozie, amesema waliomlazimisha Chika Ndubuisi au kula njama ili mwanamke huyo anywe maji yaliyotumika kuosha mwili wa mumewe ni kinyume cha sheria.
Anozie alieleza kuwa Sheria ya Kuzuia Ukatili dhidi ya Watu (VAPP-Law) inaeleza adhabu kwa wanaofanya vitendo hivyo.
Pia alisema katiba ya Nigeria inataja haswa haki ya watu kudhulumiana.
Kwa hali ilivyo sasa, “wale wanaofanya vitendo hivyo wanaweza kufungwa hadi miaka mitano au kulipa faini kama adhabu”.
Sheria ya VAPP kusini mashariki mwa Nigeria
Nnenna Anozie alisema kuwa Sheria ya VAPP ilikuwa sheria iliyoanzishwa nchini Nigeria mwaka wa 2015 wakati wa utawala wa Goodluck Jonathan.
“Sheria hii inakataza aina nyingi za unyanyasaji dhidi ya wanawake, ikiwa ni pamoja na unyanyasaji unaoitwa utamaduni au jadi.”
“Kumnywesha mwanamke maji ya kuogea maiti ni miongoni mwa mambo yaliyokatazwa na sheria kwani ukiangalia suala hili, utaona maji hayo ni mabaya yaliooshewa maiti na yanatiwa kemkali nyingi zinazoweza kumuua mtu.
“Fahamu kuwa unyanyasaji unaokatazwa na Sheria ya VAPP unaweza kujumuisha mambo kama vile kupigwa, kunyima mtu chakula chake, kuwanyima vyombo vyao vya usafiri, au kumbaka mwanamke, miongoni mwa mambo mengine.”
Anozie alieleza zaidi kuwa serikali zote za kusini mashariki zimepitisha Sheria ya VAPP kuwa sheria katika majimbo yao.
Alifafanua kuwa Jimbo la Anambra lilipitisha Sheria ya VAPP kuwa sheria katika jimbo hilo mnamo 2017, Enugu mnamo 2019, Imo mnamo 2021, Ebonyi mnamo 2021 wakati Abia aliipitisha kuwa sheria mnamo 2020.