Wanajeshi wa Israel wamefanya shambulizi la nchi kavu katika mkoa wa kusini mwa Lebanon wa Nabatieh, huo ukiwa ukiukaji mwingine wa makubaliano ya kusitisha mapigano ambayo yalianza kutekelezwa karibu mwaka mmoja uliopita.

Ripoti kutoka Lebanon zimearifu kuwa msafara wa wanajeshi wa Israel uliokuwa na magari kadhaa aina ya Jeep mapema leo uliingia hadi katika mji wa mpakani wa Blida katika wilaya ya Marjayoun na kuvunja jengo la muda la manispaa ya mji huo.

Hujuma hiyo ya Israel ilifuatiwa na ndege zisizo na rubani za utawala wa Kizayuni zilizokuwa zikiruka katika mji wa Blida. Sauti za risasi zilisika pia wakati wa shambulio hilo la wanajeshi wa Israel katika mji wa Blida katika mkoa wa Nabatieh kusini mwa Lebanon.

Baada ya shambulizi hilo la nchi kavu, Manispaa ya mji wa Blida ilitangaza kuwa mfanyakazi wake aliyetambulika kwa jina la Ibrahim Salameh ambaye alikuwa ndani ya jengo hilo ameuawa na wanajeshi wa Israel katika hujuma hiyo. 

Wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wameumuuwa Salameh akiwa amelala. Jeshi la Lebanon lilifanikiwa kufika mbele ya eneo walipokuwa wanajeshi vamizi wa Israel huku askari jeshi wa ziada wakitumwa pia katika mji wa wa Blida.

Nawaf Salam Waziri Mkuu wa Lebanon amelaani vikali shambulizi la nchi kavu la wanajeshi wa Israel katika mji wa Blida na kulitaja kuwa ni shambulio dhidi ya taasisi za serikali za Lebanon na mamlaka ya kujitawala ya nchi hiyo. 

“Tuko pamoja kikamilifu na wananchi wetu wa kusini na katika vijiji vya mpakani ambao wanagharamika kwa kutetea haki yao ya kuishi kwa amani na heshima chini ya mamlala ya taifa la Lebanon,” amesema Waziri Mkuu wa Lebanon.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *