Chanzo cha picha, Getty Images
Bunge la Ulaya limesema kuwa Uchaguzi Mkuu wa Tanzania wa tarehe 29 Oktoba 2025, ”haukuwa huru na wa haki” na kuelezea kusikitishwa kwao na huo Uchaguzi Mkuu kwa ujumla.
“Tunataka washirika wa kidemokrasia kusimama kidete kutetea demokrasia na haki za binadamu,” Taarifa ya pamoja iliyotolewa na Bunge hilo imesema.
Taarifa ya Bunge hilo imedai kuwa uchaguzi huo umekumbwa na udanganyifu na kuwa mchakato huo ulianza kufanywa miezi kadhaa iliyopita.
“Watanzania walipokwenda kupiga kura, Jumuiya ya Kimataifa imefuatilia mchakato kwa masikito makubwa. Kile ambacho kingekuwa kufurahia demokrasia, badala yake kimebadilika kuwa ukandamizaji, vitisho na hofu. Uchaguzi huu haukuwa huru na wa haki. Udanganyifu haukuanza kwenye sanduku la kupigia kura,” taarifa hiyo imeongeza.
Wabunge hao wamezungumzia suala la viongozi wa upinzani kunyanyaswa na kukamatwa, vyama vyao kutengwa, na uhuru wa kujieleza kuingiliwa.
“Kukamatwa na kesi inayoendelea ya uhaini dhidi ya kiongozi wa upinzani Tundu Lissu – mtu ambaye bunge hilo imesema uhalifu wake pekee ni kudai uchaguzi huru na wa haki ni mfano wa kuporomoka kwa maadili ya kidemokrasia na uhuru wa mahakama nchini Tanzania. Bunge hilo aidha limeitaka serikali ya Tanzania kumuachilia huru Lissu bila masharti.
“Hakuna uchaguzi ambao unaweza kuwa wa kuaminika wakati chama kikuu cha upinzani kimenyamazishwa,” Taarifa hiyo imesema.
Bunge hilo limedai kuwa uchaguzi mkuu nchini Tanzania umekumbwa na dosari kutokana na kuingiliwa kwa uhuru wa kukusanyika na kujieleza huku vyombo huru vya habari vikitishwa au kudhibitiwa.
Chanzo cha picha, BBC NEWS
Katika kipindi cha miaka miwili hivi iliyopita, nafasi ya kisiasa nchini Tanzania imepungua kwa kiasi kikubwa – wakosoaji wa serikali walengwa na sauti za upinzani kunasemekana kuwa katika hali mbaya zaidi sasa, kuliko ilivyokuwa chini ya Magufuli, huku utekaji nyara na mauaji ya mara kwa mara yakiripotiwa.
“Samia aliingia kwa sauti ya maridhiano, lakini sasa amekuwa amekuwa mwenye kufanya maamuzi magumu ambayo wengi hawakutarajia kutoka kwake,” alisema mchambuzi wa kisiasa Bw Issa alipozungumza na BBC.
“Sasa analaumiwa pakubwa kwa baadhi ya mambo kama vile utekaji nyara, mauaji, ukandamizaji wa upinzani na masuala mengine kuhusu usalama.”
Hii imeakisiwa pia katika ripoti za Freedom House, shirika la utetezi wa demokrasia na haki za binadamu lenye makao yake nchini Marekani, ambalo liliiweka Tanzania kama taifa “huru kwa kiasi fulani” mwaka 2020 na “lisilo huru” mwaka jana.
Hata hivyo, serikali haijazungumzia tuhuma hizo.
Wakati tume ya uchaguzi imewaachia wagombea urais 17 kugombea urais wakati huu, chama kikuu cha upinzani Chadema kimezuiwa kushiriki uchaguzi huku kiongozi wake Tundu Lissu akikabiliwa na kesi ya uhaini.
Alikuwa akitoa wito wa mageuzi ya uchaguzi kabla ya kukamatwa kwake mnamo mwezi Aprili.
Makamu wake, John Heche, naye alikamatwa wiki chache zilizopita – na aliiambia BBC kabla tu ya kuwekwa kizuizini kwamba kile kinachoitwa mageuzi ya Rais Samia ni mambo yasio na msingi: “Ndiyo, mikutano ya hadhara iliruhusiwa tena, lakini leo Chadema haiwezi kutekeleza wajibu wake kwa sababu ahadi zilikuwa za uongo.”
Wakati huo huo, mgombea urais Luhana Mpina, kutoka chama cha pili kwa ukubwa cha upinzani, ACT Wazalendo, pia alienguliwa – mara mbili.
Alifaulu kurejeshewa ugombeaji wake na Mahakama Kuu baada ya kuzuiliwa kutokana na suala la kiutaratibu – lakini Mwanasheria Mkuu wa Serikali alikata rufaa mwezi uliopita na tume ya uchaguzi iikaamua kuunga mkono upande wake.

Wakati shughuli za kura kuhesibiwa ikiwa inaendelea nchini Tanzania, Bunge la Ulaya limetoa wito wa “kuhimiza washirika wote wa Kidemokrasia kusimama kidete katika utetezi wa demokrasia na haki za binadamu. Ukimya sio sawa na kutoegemea upande wowote – ni kufanya mambo kuwa mugumu zaidi.”