
Msemaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas, amelalamikia vikali visingizio vya uongo vinavyotumiwa na utawala vamizi wa Kizayuni vya kujaribu kuhalalisha jinai zake dhidi ya raia wa Palestina na kusema kuwa huo ni ushahidi wa ubaguzi wa rangi na chuki za kupindukia walizo nazo Wazayuni dhidi ya wanawake na watoto wa Palestina waliouliwa kikatili na kwa umati na mwanajeshi makatili wa Kizayuni.
Hazem Qassem, msemaji wa Hamas aidha amesema kwamba, njama zinazofanywa na utawala vamizi na muuaji wa raia wasio na ulinzi katika Ukanda wa Ghaza, kwa kisingizio kwamba mashambulizi ya wanajeshi yalikuwa ni ya kujihami, ni madai ya uongo na ni kielelezo cha ubaguzi wa rangi na chuki zisizo na kifani za Wazayuni dhidi ya raia wa Palestina.
Aidha amesisitiza kwa kusema: Haikubaliki kabisa kudai kwamba mauaji ya raia zaidi ya 100 wa Palestina, ambao wengi wao walikuwa ni wanawake na watoto wasio na ulinzi yamefanyika kwa ajili ya kujihami mwanajeshi wa Kizayuni, na dunia inawezaje kuhalalisha uhalifu na jinai kama hiyo kwa kisingizio chochote kile?
Ameongeza kuwa, kauli za afisa wa Marekani aliyejaribu kuhalalalisha jinai na ukatili wa Israel kwa kudai kuwa utawala wa Kizayuni umetoa “jibu dogo tu” na ilikusudia kushambulia wanachama wa harakati ya Hamas zinakinzana na ukweli uliothibitishwa rasmi wa kuuawa shahidi watoto 46 na wanawake 20 tena katika kipindi cha usiku mmoja tu.
Wazayuni wamekuwa wakikanyaga mara kwa mara makubaliano ya kusimamisha vita Ghaza tangu mwanzoni kabisa mwa kutiwa kwake Saini. Hadi hivi sasa wameshaua idadi kubwa ya raia kwa visingizio visivyokubalika kama vile kudai HAMAS inachelewesha kwa makusudi kukabidhi maiti za Wazayuni wakati mateka hao waliuliwa na wanajeshi wenyewe wa Israel na wamefukiwa kwenye vifusi vya majengo yaliyobomolewa na makombora ya utawala wa Kizayuni. HAMAS wanasema itachukua muda kuweza kuipata miili ya Wazayuni hao.
