
Rais wa Uturuki amekosoa vikali msimamo wa Ujerumani wa kuuunga mkono utawala wa Israel, akimwambia kansela wa nchi hiyo: “Je, huoni mauaji ya halaiki na njaa ya kutengeneza kwa makusudi inayowakabili watu wa Gaza?”
Shirika la habari la Anadolu limeripoti kuwa, akiwa katika mkutano wa pamoja wa waandishi wa habari na Kansela wa Ujerumani Friedrich Meretz, Recep Tayyip Erdogan amesisitiza udharura wa kukomeshwa mara moja vitendo vya utawala wa Israel, na kuongeza kuwa Tel Aviv inaendeleza vita vya mauaji ya kimbari na kuwasababishia njaa watu wa Palestina.
Ameashiria mauaji ya watoto, wanawake na wazee takriban 60,000 katika mashambulizi ya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya watu wa Gaza na kusema: “Hamas haina mabomu wala silaha za nyuklia, lakini Israel ina haya yote, na jana usiku iliishambulia tena Gaza kwa mabomu.”
Erdogan ametoa wito wa ushiriki hai wa Ujerumani, Uturuki na nchi za kikanda katika kukomesha mauaji ya kimbari ya utawala wa Kizayuni dhidi ya watu wa Gaza na kujenga upya eneo hilo, akisisitiza kwamba hili ni jukumu la pamoja la kibinadamu.
Rais wa Uturuki amemwambia Kansela wa Ujerumani kwamba: “Kama ambavyo tunataka kukomeshwa vita nchini Ukraine, vivyo hivyo tunapaswa kutaka kukomeshwa vita huko Gaza, na Uturuki na Ujerumani zinaweza kuwa na nafasi muhimu katika kufikiwa lengo hili.”