Chanzo cha picha, Twitter/@SuluhuSamia
-
- Author, Asha Juma
- Nafasi, BBC Nairobi
“Namtangaza Samia Suluhu Hassan kuwa rais mteule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chama cha CCM,” Tangazo la mwenyekiti wa INEC, Jacobs Mwambegele asubuhi ya Jumamosi, 01/11/2025.
Unaweza kuyaona maneno ya kawaida kwako lakini ndio ambayo yametoa mwelekeo wa nchi ya Tanzania baada ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu 20/10/2025 na kumpa Samia Suluhu Hassan fursa ya kuendelea kuwa madarakani kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.
Samia Suluhu Hassan ameibuka mshindi kwa kupata 31,913,866 kati ya 32,678,844 kura zilizopigwa – zaidi ya aslimia 97.
Lakini je, Samia Suluhu Hassan ni nani haswa?
Samia alizaliwa mwaka 1960, amepata fursa ya kuwa rais wa sita wa Tanzania na anatokea visiwani Zanzibar.
Ni rais wa pili wa Tanzania kutokea Zanzibar, wa kwanza akiwa Mzee Ali Hassan Mwinyi aliyeliongoza taifa hilo kwa miaka 10 kutoka mwaka 1985 mpaka 1995.
Samia ni msomi wa kiwango cha shahada ya uzamili kutoka chuo kikuu cha Manchester nchini Uingereza.
Pia alipata fursa ya kusomea chuo kikuu cha Southern New Hampshire kupitia programu ya ushirikiano na chuo cha Open University cha Tanzania.
Mnamo mwaka 1988, Suluhu alikua afisa wa maendeleo na serikali ya mkoa wa Zanzibar. Akawa meneja wa mradi wa shirika la chakula duniani (WFP) Zanzibar.
Miaka ya 1990, alipewa jukumu la kusimamia mashirika yasiyokuwa ya kiserikali huko Zanzibar.
Safari ya Samia kisiasa
Chanzo cha picha, Getty Images
Mnamo mwaka 2000, Suluhu alikua mwanachama wa kiti maalum cha Baraza la Wawakilishi la Zanzibar na Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambapo aliteuliwa Waziri wa Zanzibar wa Ajira ya Vijana, Wanawake na watoto.
Wakati akiwa katika nafasi hii, alimaliza marufuku kwa akina mama waliopata watoto kwa mara ya kwanza kurudi shuleni.
Aliteuliwa tena mwaka 2005 na kuwa Waziri wa Utalii na Biashara.
Mnamo mwaka wa 2010, Suluhu aligombea ubunge katika jimbo la Makunduchi na kushinda kwa zaidi ya 80%. Rais Jakaya Kikwete alimteua kama Waziri wa Nchi wa Masuala ya Muungano.
Samia aliingia madarakani mnamo 2021 kufuatia kifo cha mtangulizi wake hayati Rais John Pombe Magufuli.
Akiwa chini ya Magufuli, Samia alikuwa Makamu wa Rais toka mwaka 2015 na kumfanya kuwa mwanamke wa kwanza kushika wadhifa huo nchini Tanzania.
Safari ya Samia katika siasa ilianza kitambo kidogo lakini kutangazwa kwake kama Rais Mteule wa Tanzania katika Uchaguzi wa 2025, kunaweka rekodi mpya ya kushika nyadhifa ya juu zaidi nchini humo na pia Afrika Mashariki kama mwanamke wa kwanza kuchagulia kuwa rais.
Kwa Watanzania wengi Samia alipata umaarufu zaidi alipoteuliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Bunge la Katiba lililoteuliwa mwaka 2014.
Tanzania ilikuwa inaelekea kutengeneza Katiba mpya – baada ya kukamilika kwa kazi ya kukusanya maoni ya wananchi kupitia Tume ya Jaji Warioba na Mama Samia alikuwa amepewa jukumu la kuongoza mchakato huo kupitia Bunge la Katiba.
Kwa sababu bunge lile lilikuwa likionyeshwa moja kwa moja kupitia vituo mbalimbali vya runinga na Watanzania wengi wakiwa na kiu kubwa ya kujua nini kinaendelea – sura ya Samia ilianza kuzoeleka kwenye macho ya wengi na uwezo wa kuongoza ukionekana dhahiri.
Lakini hiyo ilikuwa taswira yake ya hadharani. Akiwa bungeni wakati ule, Samia alikuwa akifahamika kwa uwezo wa kuonyesha utulivu – hata katika nyakati ambazo hali ya hewa katika bunge hilo imechafuka.
Muundo wa bunge hilo ulitaka viongozi wake wa juu watoke katika pande mbili za muungano na kwa vile mwenyekiti wa bunge hilo alikuwa ni hayati Samuel Sitta kutoka Tanzania Bara, nafasi ya Makamu Mwenyekiti iliangukia kwa Mzanzibari Samia.
Hata hivyo, wengi hawakutarajia kwamba angetangazwa na aliyekuwa mgombea urais wa chama cha mapinduzi mwaka 2015, John Magufuli, kuwa mgombea mwenza wake kwenye uchaguzi huo.
Ingawa wakati huo tayari alikuwa na uzoefu wa uwaziri wa takribani miaka 15; kujumlisha na uzoefu wake katika Bunge la Katiba- si watu wengi walimwona yeye kama mmoja wa watu wanaoweza kupewa wadhifa huo.
Alipoingia madarakani, wengi walimwogopa kwa sababu ya heshima yao kwake – lakini kuvunja mipaka, akaomba jambo moja kwao; wamwite Mama.
Suluhu pia, alionekana kubadilisha misimamo iliyokuwa inashikiliwa na mtangulizi wake John Pombe Magufuli.
Kama rais, Samia ametumia sera za kupunguza kuenea kwa janga la Covid-19 nchini Tanzania na kuruhusu kuingia kwa chanjo za ugonjwa huo, ambalo mtangulizi wake John Magufuli alikuwa amelipuuza.
Aidha, aliendeleza miradi iliyokuwa imeanzishwa na Rais Magufuli na kunadi Tanzania kimataifa hasa katika sekta ya utalii.
Vile vile, Samia aliruhusu uhuru wa kujieleza na kufanya mikao na viongozi wa upinzani tofauti na ilivyokuwa nyuma.
Kuruhusu mikutano hii ilikuwa mojawapo ya mambo aliyoshauriwa kufanya na wadau mbalimbali wa siasa za Tanzania.
Akihojiwa kama mchambuzi, Ezekiel Kamwaga alisema… “mikutano hii itatoa fursa kwa watu kusema yaliyo moyoni mwao. Katika Uyunani ya kale, haki ya watu kutoa maoni ilijulikana kama ‘Forum internum’, ikimaanisha fursa hiyo humpa mtu kuzungumza kile kilichomjaa moyoni mwake. Si kila kitakachosemwa na kuzungumzwa, kitamfurahisha kila atakayeona na kusikia.”
Na kama Kamwaga alivyotabiri, huu ndiyo umekuwa mtihani mkubwa zaidi kisiasa kwa utawala wa Rais Samia.
Katika miaka ya hivi karibuni, mashirika ya kutetea haki za kibinadamu, yamekashifu uongozi wake kwa madai ya utekaji, kuiwekea upinzani vikwazo ambavyo ni pamoja na kuwakamata wapinzani, na kuwazuia kushiriki katika uchaguzi mkuu.
Hata hivyo, rais huyo ameagiza kuchunguzwa kwa madai ya utekaji na pia kuahidi katiba mpya.
Siri ya mafanikio ya Samia
Chanzo cha picha, Twitter/@SuluhuSamia
Sifa moja kubwa ambayo watu waliowahi kufanya naye kazi wanaisema na ambayo si watu wengi wa nje wanaifahamu ni uwezo wake mkubwa wa kiuongozi.
Mbunge wa jimbo la Bumbuli (CCM), January Makamba, anasema Samia ni miongoni mwa wanasiasa wenye uwezo mkubwa aliowahi kufanya kazi nao na ni bahati mbaya tu kwamba wengi wa Watanzania hawajapata fursa ya kuliona hilo.
Makamba alifanya kazi kwa karibu na mama Samia katika kipindi cha kati ya mwaka 2015 hadi 2020 wakati akiwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais – ambapo alikuwa akiripoti kwa mama huyo moja kwa moja.
“Mama Samia amedunishwa. Ana uwezo mkubwa wa kufanya aonekane ni mwanasiasa wa kawaida lakini ukweli ni kwamba uwezo wake ni mkubwa sana na hili sijasimuliwa na mtu bali nimeliona kwa kufanya naye kazi kwa karibu,” alisema.
Mama Samia anaelezwa kama mwanasiasa anayependa kufanya maamuzi kupitia kusikiliza kila mmoja na si mtu wa kuamua mambo kwa pupa au kwa kuonea wengine.
Samia pia anaelezwa kuwa mwanasiasa jasiri na asiyeyumbishwa kwenye jambo analoliamini na kulikuwa na maneno kwamba uamuzi wa Kamati Kuu ya CCM kumfanya yeye kuwa mgombea mwenza wa Magufuli kwenye uchaguzi wa mwaka 2015 kulitokana pia na kufahamu sifa yake hiyo.
Kwa vile Magufuli ni mtu anayeamini katika kusukuma mambo kwa haraka na wakati mwingine bila kujali athari za kisiasa au kisaikolojia kwa uamuzi huo, CCM ilitaka Makamu atakayekuwa na uwezo wa kumwambia ukweli bila kumwogopa badala ya kukubali kila kitu.
Mfano mmoja wa tabia za Samia ni kitendo chake cha kwenda kumjulia hali aliyekuwa Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, alipokuwa amelazwa nchini kenya.
Katika mojawapo ya matukio ya kutisha kwenye historia ya Tanzania, Lissu alishambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana Septemba mwaka 2017 akiwa jijini Dodoma alikokuwa anahudhuria vikao vya bunge.
Samia alikuwa ndiye kiongozi wa juu wa kwanza wa serikali – na pekee, kwenda kumuona mwanasiasa huyo mashuhuri.
”Safari yangu haijakuwa rahisi”
Mama Samia aliolewa na mumewe, Hafidh Ameir, mnamo mwaka 1978 na katika ndoa yao wamejaliwa kupata watoto wanne.
Mtoto wake maarufu zaidi – Wanu, ni mbunge wa bunge Tanzania.
Bi Samia anasema kuwa njia yake ya ufanisi haijakuwa rahisi kama inavyodhaniwa.
”Safari yangu katika siasa imekuwa njia ndefu na yenye tija. Sio rahisi kuwajibikia familia yako wakati huohuo ukiendelea na maisha ya siasa, elimu na majukumu mengine ya kikazi,” anasema Bi Samia.