
Ofisi ya Vyombo vya Habari ya Ghaza imetangaza kwamba jeshi vamizi la Israel limeshakanyaga mara 194 makubaliano ya kusitisha vita huko Ghaza yaliyofikiwa tarehe 10 Oktoba kwa ajili ya kumaliza mauaji ya kimbari ya miaka miwili yaliyokuwa yanafanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya wananchi wa Ghaza.
Kwa mujibu wa ofisi hiyo, jeshi la Israel limeshakanyaga mara 194 makubaliano ya usitishaji mapigano katika Ukanda wa Ghaza tangu yalipoanza kutekelezwa tarehe 10 mwezi uliopita wa Oktoba.
Mkurugenzi wa ofisi hiyo, Ismail al-Thawabta ametangaza habari hiyo na kuongeza kwamba, ukiukaji huo wa makubaliano ya kusitisha vita unajumuisha pia kupenya vikosi vya Israel ndani zaidi ya kile kinachoitwa “Mstari wa Njano” pamoja na vitendo vya utawala wa Kizayuni vya kuzuia kuingia dawa, vifaa vya matibabu, mahema na nyumba zinazohamishika kwenye Ukanda wa Ghaza mbali na mashambulizi ya jeshi la Israel kwa kutumia risasi na makombora pamoja na kuvamia baadhi ya maene ya Ghaza.
Kwa mujibu wa al-Thawabta, vikosi vya Israel vinavuka mara kwa mara “Mstari wa Njano” na kuingia katika maeneo ya makazi ya raia na maegesho ya magari, vikifanya mashambulizi ya anga na kubomoa maeneo ya Wapalestina na kuwasababishia vifo na majeraha raia.
Mkurugenzi wa Ofisi ya Vyombo vya Habari ya Ghaza amewataka Wapalestina wasikaribie eneo liitwalo “Mstari wa Njano” kwani wanaweza kupigwa risasi na wanajeshi wa Israel bila ya hata kuonywa. Amekumbusha kwamba Israel tangu zamani imekuwa ikiua raia waliokwenda kutembelea nyumba zao karibu na eneo hilo.
Ofisi ya Vyombo vya Habari ya Ghaza imetangaza pia kwamba makubaliano ya kusitisha mapigano yanajumuisha kifungu kinachoruhusu kuingia Ghaza mamia ya magari mazito ili kutoa miili ya wahanga wa vita kutoka kwenye vifusi lakini Israel inakwamisha jambo hilo.