
Rais Felix Tshisekedi wa DRC amesema kuwa, mazungumzo ya amani kati ya serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na kundi la waasi la Machi 23 (M23) yataanza tena wiki ijayo huko Doha, mji mkuu wa Qatar.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Jumapili jioni na Ikulu ya Kinshasa, Rais Tshisekedi amethibitisha tena kwamba DRC bado imejitolea kutatua migogoro wa nchi hiyo kwa njia za kisiasa na kidiplomasia ili kumaliza mgogoro katika majimbo ya mashariki mwa nchi sambamba na kuendelea kulinda uhuru na kujitawala ardhi yote ya DRC.
Doha imeendelea kuwa eneo pekee la kufanyia mazungumzo kati ya Kinshasa na waasi wa M23 kwa miezi kadhaa. Mwezi Julai mwaka huu, Kinshasa na waasi wa M23 walitia saini azimio maalumu huko Doha ambalo ni ramani ya njia ya makubaliano ya kutatua mgogoro wa DRC.
Rais Tshisekedi, ambaye aliwasili Doha mji mkuu wa Qatar jana Jumapili kwa ajili ya kushiriki Mkutano wa Pili wa Kimataifa wa Maendeleo ya Jamii uliopangwa kufanyika Novemba 4 hadi Novemba 6, amemshukuru Amir wa Qatar, Sheikh Tamim bin Hamad Aal Thani kwa kusimamia mazungumzo yanayoendelea kati ya serikali ya Kinshasa na waasi wa M23.
Baada ya kuibuka tena waasi wa M23 mwishoni mwa mwaka 2021, waasi hao wameweza kuteka maeneo mengi ya mashariki mwa DRC huku Kinshasa ikiishutumu moja kwa moja Rwanda kwa kuwaunga mkono waasi hao. Baada ya waasi wa M23 kuungana na makundi mengine na kuunda muungano wa kisiasa na kijeshi wa Fleuve Congo (AFC), wamefanikiwa kudhibiti miji muhimu na maeneo ya kimkakati mashariki mwa DRC, ikiwa ni pamoja na miji mikubwa na muhimu ya Goma na Bukavu.