Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Sayyid Abbas Araghchi amesema kwamba Jamhuri ya Kiislamu imejiandaa zaidi kwa vita hivi sasa kuliko hata ilivyokuwa kabla ya vita vya siku 12 akisisitiza kwamba Tehran haiziamini ahadi za Israel wala Marekani lakini iko tayari kwa mazungumzo ya kiuadilifu yaatakayolinda haki zake zote za nyuklia.

Sayyid Araghchi amesema hayo katika mahojiano maalumu aliyofanya jana na televisheni ya Al Jazeera ya Qatar ambayo yalijadili mambo mbalimbali kama vile vita vya hivi karibuni kati ya Iran na Israel, kadhia ya nyuklia na uhusiano mgumu na madola ya Magharibi.

Waziri Araghchi amesema kwamba vita vya hivi karibuni vya siku 12 vilifichua uwezo wa Iran wa kujihami na vilitoa fursa nzuri ya kufanyiwa majaribio ya kweli makombora ya Iran na mifumo ya ulinzi ya Jamhuri ya Kiislamu. 

Amesema, “Iran imepata uzoefu mkubwa wa kijeshi na kiufundi kutokana na vita hivyo, imepata fursa ya kufanyia majaribio makombora yake katika vita halisi na kuthibitisha kivitendo kwamba mifumo ya ulinzi ya Israel inapenyeka.”

Ameongeza kuwa kujiandaa kijeshi Iran hivi sasa kumefikia kiwango kisicho cha kawaida, akielezea imani yake kwamba “Israeli haitothubutu kuanzisha tena vita, kwa sababu inajua kwamba jibu la Iran litakuwa kali zaidi.” Wakati huo huo amesema kuwa Tehran inayachukulia kwa uzito unaostahiki masuala yote na imejiandaa vilivyo kukabiliana na uchokozi wowote na wala haiziamini ahadi za Israel na Marekani. 

Araghchi vilevile amesema kwa kujiamini kwamba, mashambulizi ya Marekani dhidi ya vituo vya nyuklia vya Iran yalishindwa kufikia malengo yake, akisisitiza kwamba Jamhuri ya Kiislamu haijapoteza utaalamu na ujuzi wake wa nyuklia suala ambalo linazifanya shughuli zake za nyuklia kuendelea kwa nguvu licha ya Marekani kushambulia vituo vyake vya nyuklia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *