Baadhi ya marsharti yaliotangazwa nchini Tanzania wakati wa uchaguzi ikiwemo kukatwa kwa intaneti na marufuku ya watu kutembea yameanza kuondolewa.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Dakika 2 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Tume ya uchaguzi katika taifa hilo la Afrika Mashariki ilimtangaza Rais Samia Suluhu Hassan kuwa mshindi wa uchaguzi mkuu wa Oktoba 29 kwa kupata asilimia 98 ya kura zote zilizopigwa.
Licha ya tangazo hilo la tume ya uchaguzi, upinzani ulitupilia mbali matokeo yenyewe.
Watanzania wamekosa intaneti tangu kuzuka kwa maandamano siku ya uchaguzi ila kufikia sasa baadhi ya maeneo yamekuwa yakiripoti kupatikana kwa huduma hiyo.

Licha ya baadhi ya wakazi kuripoti kuanza kurejeshwa kwa mfumo wa intaneti, bado inasalia vigumu kuthibitisha baadhi ya habari kutoka nchini humo.
Kando na kurejeshwa kwa huduma za intaneti, mpiga picha wa shirika la habari la AFP amethibitisha kuanza pia kurejelewa kwa shughuli za kawaida katika jiji kuu la kibiashara Dar es Salaam siku ya Jumanne licha ya watu kuendelea kusalia na uwoga.
“Natumai machafuko hayatatokea tena,” muchuzi wa chakula Rehema Shehoza, 32, ameiambia AFP.
“Wengi wetu tunaweza tukafaa kwa njaa kwa sababu nahitaji kufanya kazi kupata makate wangu wa kila siku,” alisema.

Siku ya Jumatatu ya wiki hii polisi walitangaza kufuta makataa ya watu kutembea nje yaliokuwa yametangazwa siku ya uchaguzi.
Baadhi ya magari ya uchukuzi wa umma yameonekana yakiendeleza shughuli zake baada ya uchukuzi kutatizika kwa muda.
AFP pia imeripoti kuendelea kuimarishwa kwa usalama jijini Dar es salaam japokuwa idadi ya maofisa wa polisi imeendelea kupungua.
Baadhi ya picha na video zinazodaiwa zilipigwa na waandamanaji wakati wa vurugu za uchaguzi zimeanza pia kuchapishwa, hatua inayotajwa kuonyesha mfumo wa intaneti umeanza kurejea.

Jumatatu ya wiki hii, polisi ilichapisha ujumbe ikitishia kuwaadhibu watu watakao sambaza video zinazoweza kuchochea wasiwasi au kuwadhalilisha watu mitandaoni.
Chanzo cha kidiplomasia kilisema kuwa kulikuwepo na taarifa za uhakika za kutokea kwa vifo vya mamia ya watu wakati wa machafuko yalioshuhudiwa siku ya uchaguzi na baada ya uchaguzi wenyewe.
Chama kikuu cha upinzani Chadema kiliambia AFP kuwa kilirekodi zaidi ya vifo 800 kufikia Jumamosi ya wiki iliopita japokuwa takiwimu hizo hazingeweza kuthibitika.