
Watu zaidi ya 30 wamepoteza maisha katika jimbo la Niger, nchini Nigeria, baada ya boti waliyokuwa wanasafiria kuzama kwenye mto Malale.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Wakati boti hiyo ikizama, ilikuwa na abiria karibu 100, wakiwemo wanaume, wanwake na watoto, kwa mujibu wa ripoti za maafisa wa serikali katika jimbo hilo.
Mwakilishi wa Shirika la Msalaba Mwekundu, Abubakar Idris, amesema chanzo cha ajali hiyo ni boti hiyo kubeba abiria kupita kiasi na kugongana na kisiki cha mti.
Watu wengine zaidi ya 50 waliokuwa kwenye boti hiyo, wameokolewa lakini wengine wanane, bado hawajulikani walipo, huku maafisa wa msalaba Mwekundu wakisema, zoezi la uokoaji linaendelea.
Abiria, hao walikuwa wanasafiri kutoka jiji cha Dugga, kwenda kwenye kijiji jirani kilicho umbali wa Kilomita karibu 20 kwenda kuhudhuria mazishi ya mpendwa wao.
Mwezi Agosti, boti nyingine iliyokuwa na abiria 50, ilizama kwenye jimbo la Sokoto na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 20.
Ajali kama hizi ni kawaida katika mito mbalimbali nchini Nigeria, na sababu kubwa imekuwa abiria kupita kiasi, vifaa vya usafiri wa majini kutofanyiwa ukarabati na wamiliki kutozingatia taratibu za usalama.