WANANCHI wakiwemo viongozi wa dini wametoa mwito kwa wananchi kuipenda nchi yao na kulinda amani kwa kuzingatia falsafa ya 4R inayomaanisha ya Maridhiano, Ustahimilivu, Mageuzi na Kujenga upya.
Katibu wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT), Askofu Israel Maasa alisema ni muhimu kutekeleza kwa vitendo falsafa ya 4R.
Askofu Maasa alilieleza gazeti la HabariLEO falsafa hiyo ni tiba kwa yaliyotokea katika Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani.
SOMA: Watanzania tusimamie misingi, utu wema kulinda amani ya nchi
“Si lazima yote yatakayoongelewa yakubaliwe. Tunaweza kukubaliana katika kutokukubaliana kwa amani, tunahitaji diplomasia zaidi katika hili,” alisema.
Kwa upande wake, Katibu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) mkoani Kilimanjaro, Awadh Lema alisema ni muhimu wananchi kufundishwa uzalendo.
Naye Askofu wa makanisa ya PMC Tanzania, Gervase Masanja alisema ni muhimu viongozi wa dini waelimishe waumini waombe amani na utulivu.
Askofu Masanja alilieleza HabariLEO ofisini kwake Kibaha mkoani Pwani kuwa ni muhimu kuendeleza mshikamano ili nchi ipate utulivu na watu waendelee na shughuli za kimaendeleo.
“Falsafa ya 4R inapaswa kupewa nafasi kwani nchi itakuwa salama na iwe ajenda ya kitaifa, kwani imegusa kila eneo. Hivyo, ikitumika itasaidia watu kudumisha amani, utulivu na mshikamano wa nchi yetu,” alisema.
Aliongeza: “Cha kufanyika kwa sasa ni watu kuliombea taifa kupitia imani zao kwa kushirikiana na viongozi wao ili nchi iweze kurudi kwenye hali yake ya zamani. Wasikubali kugawanywa ili kulinda amani ya nchi, kwani hatuna Tanzania nyingine.”
Kwa upande wake, Katibu wa Msikiti wa Hadhara Raji Mzimuni Maili Moja Kibaha, Mahamudu Mudihiri alisema msingi wa maendeleo unatokana na amani.
Naye Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Mkoa wa Pwani, Abdala Ndauka alisema falsafa ya 4R itolewe kama waraka ili viongozi na wananchi waweze kuitumia.
Ndauka alisema falsafa hiyo imegusa masuala muhimu ya ustawi wa jamii na kiongozi asiyeitekeleza anapaswa ajitathmini, kwani atakuwa ameshindwa kutekeleza maelekezo ya rais.
“Cha kufanyika ni mafundisho ya watu kulinda amani utulivu na kuwa na mshikamano ili nchi iweze kujiletea maendeleo, kwani msingi wa maendeleo ni amani,” alisema.
Naye Mkurugenzi wa asasi isiyo ya kiserikali ya maendeleo ya vijana ya Kibaha (YPC), Israel Ilunde alisema huu ndiyo wakati wa kutumia falsafa ya 4R.
Ilunde alisema falsafa hiyo inajibu maswali mengi ndani ya nchi na ikitumika vizuri, mambo yataenda vizuri na
wananchi watakuwa kwenye utaratibu mzuri na kujiletea maendeleo.
Kwa upande wake, mwanasiasa mkongwe mkoani Arusha, Modesti Meikoki alishauri Watanzania waipende nchi yao na rasilimali zake.
Imeandikwa na Veronica Mheta (Arusha), John Mhala (Arusha), Heckton Chuwa (Moshi), John Gagarini (Kibaha).
