GEITA: WAKALA wa Huduma za Barabara Mjini na Vijijini Tanzania (TARURA) imetoa muda wa fidia ya makubaliano ya siku 100 kwa mkandarasi wa Mradi wa Uboreshaji wa Miji (TACTICS) mjini Geita.
Mkataba wa awali wa mradi wa TACTICS mjini Geita ulikuwa ni miezi 15 sawa na siku 458 ambapo ulianza kutekelezwa Novemba 20, 2023 na ulitarajiwa kukamilika Februari 19, 2025.
Mhandisi Mshauri wa Mradi, Mhandisi Rechnold Manyanga ametoa taarifa hiyo mbele ya mkuu wa mkoa wa Geita alipotembelea maendeleo ya mradi huo wa barabara ya Km 17 za lami.
Mhandisi Manyanga amesema mradi huo unaotekelezwa na kampuni ya Sichuan Road and Bridge (Group) Corporation LTD umeshindwa kukamilika kwa wakati na mpaka sasa umefikia asilimia 61.
Amesema kabla ya muda wa fidia, mkandarasi aliongezewa siku 250 sawa na miezi 8.4 huku matarajio hadi sasa yalikuwa ni kukamilisha mradi kwa asilimia 95 lakini mkwamo ni asilimia 34.

“Mkandarasi ameshaarifiwa kwa barua na utekelezaji umeanza Novemba 01, 2025 na utamalizika Februari 08, 2025 ambapo mkandarasi anatakiwa awe amemaliza kazi” amesema.
Mhandisi Manyanga amesema gharama za jumla za mradi ni kiasi cha sh bilioni 22.23 ambapo mkandarasi ameshalipwa jumla ya kiasi cha sh bilioni 8.06 kwa malipo ya kazi zilizothibitishwa.
“Changamoto za mradi ni uchelewaji wa uletwaji wa vifaa, upungufu wa raslimali na ufanisi wa vifaa, kuchelewa kwa kuletwa mitambo mikubwa ya usagaji kokoto na lami ndani ya muda.
“Mkandarasi ameshindwa kumaliza kazi ndani ya mud awa mkataba licha ya kuongezewa mud awa takribani miezi nane, kukaa vikao vya juu na kushauriwa kuongeza raslimali zaidi” amesema.
Mkuu wa mkoa wa Geita Martine Shigela amesema kuwa dhamira ya serikali ya awamu ya sit ani kuhakikisha inatekeleza kwa vitendo ahadi zote ikiwemo uboreshaji wa miundombinu.
“Ukiangalia kazi iliyobakia ni kubwa zaidi ya muda uliobakia, maana ametumia zaidi ya miaka miwili, ameshindwa kutimiza wajibu wake sidhani ka a siku 100 zinatosha kukamilisha kazi”, amesema.
Amesema ili kufanikisha ukamilishaji wa mradi huo halmashauri ya manispaa isimamie kuhakikisha mkandarasi anaongeza masaa ya kazi kutoka nane hadi 14 kwa siku na ufuatiliaji uimarishwe.