Wahamiaji 38 Wakamatwa MbeyaWahamiaji 38 Wakamatwa Mbeya

JESHI la Polisi mkoani Mbeya linawashikilia watu 38, wakiwemo raia mmoja wa Ethiopia, kwa tuhuma za kuingia nchini kinyume cha sheria.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Benjamin Kuzaga, amesema watuhumiwa hao walikamatwa Novemba 11, 2025 katika Pori la Ranchi ya Matebete lililopo Kijiji cha Igumbilo Shamba, Kata ya Chimala, Wilaya ya Mbarali, mkoani humo.

Kamanda Kuzaga alibainisha kuwa watuhumiwa walikuwa wakisafiri kwa gari lenye namba za usajili T.953 DJF, aina ya Toyota Noah, mali ya Stanslaus Mazengo (51) mkazi wa Isitu, ambaye pia ndiye alikuwa dereva wa gari hilo. SOMA: Kutangazwa mshindi hadi kuapishwa Rais wa Tanzania

Ameongeza kuwa katika mahojiano, mtuhumiwa Mazengo alieleza kuwa alikuwa akiwapeleka wahamiaji hao kufikishwa na kuhifadhiwa katika nyumba ya Jackline Malya (26), mkazi wa Chimala. “Watuhumiwa walikuwa wakisafirishwa kwa njia ya kificho kwa lengo la kuwavusha hadi nchini Afrika Kusini,” alisema Kamanda Kuzaga.

Aidha, ametoa rai kwa wananchi kuacha tamaa ya fedha na kuacha kushiriki katika biashara haramu ya kuwawezesha raia wa kigeni kuingia au kupita nchini bila kibali.“Wananchi wanapaswa kuwaelekeza wageni kufuata taratibu za kisheria kupitia mamlaka husika ili kuepuka usumbufu na adhabu za kisheria,” alisisitiza Kamanda Kuzaga.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *