KUTOKUTUMIKA ipasavyo kwa miundombinu ya kisasa kwenye masoko yanayomilikiwa na Manispaa ya Kinondoni iliyopo Dar es Salaam kunasababisha upotevu mkubwa wa mapato.

Kama masoko hayo yangetumika ipasavyo, yangeingiza mabilioni ya fedha.

Uchunguzi uliofanywa na Dailynews Digital kwa takribani miezi mitatu katika masoko matatu ya kisasa ya Magomeni, Tandale na Bwawani unaonesha kuwa, masoko hayo bado hayajatumika kama ilivyopangwa wakati wa mikakati ya ujenzi wake.

Masoko hayo yamejengwa kwa fedha za Serikali Kuu Sh bilioni 22.2.

Soko la Magomeni liligharimu Sh bilioni 10.5, Soko la Bwawani Sh bilioni 1.5 na Soko la Tandale Sh bilioni 10.2.

Huduma zote zinazohitajika vikiwemo vyoo vya kisasa, lifti, maegesho, maji safi na ngazi katika masoko hayo yenye maghorofa yasiyozidi matatu zinapatikana.

DailyNews Digital ilipotembelea masoko hayo, ilishuhudia kutotumika kwa maeneo mengi katika masoko ya Magomeni na Tandale huku vizimba, fremu na maeneo mengine yakibaki na vumbi.

Kwa Soko la Magomeni eneo la ghorofa juu, walionekana wafanyabiashara wachache wakiyatumia kama sehemu ya uchuuzi wa samaki, maduka machache ya dawa asili, ukumbi na eneo la kufanyia mazoezi.

Imenabinika kuwa, wafanyabiashara wengi wanakwepa kutumia maeneo hayo na kuonekana nje ya soko hilo la kisasa wakiwa wameweka mabanda chakavu.

Kadhalika katika Soko la Tandale, ni eneo la chini pekee linalotumika huku ghorofa ya kwanza na ya pili maeneo yote yakiwa hayana wafanyabiashara wala shughuli nyingine.

Pembeni mwa barabara kumeshuhudiwa kukiwa na wafanyabiashara mbalimbali.

Katika Soko la Bwawani, ukarabati wa kubadilisha matumizi ya soko hilo kuwa Kituo cha kuuza bidhaa za urembo na upambaji umeshuhudiwa kuendelea.

Kwa mujibu wa Ripoti ya Mkaguzi Mkuu na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG), Ripoti Kuu ya Mwaka ya Ukaguzi wa Serikali Kuu kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 masoko hayo yaliyokamilishwa ndani ya Mamlaka ya Halmashauri ya Kinondoni hayajatumiwa ipasavyo.

Ripoti hiyo inathibitisha Soko la Magomeni sehemu limetekelezwa tangu mwaka 2022. Soko la Tandale limebaki bila kutumika licha ya lengo la ukusanyaji wa mapato ya Sh milioni 500.1 kwa Mwaka wa Fedha 2023/24 ambapo sasa limeingiza Sh milioni 120 kwa mwaka .

Katika mahojiano, wafanyabiashara wa masoko hayo wanasema hali ngumu ya biashara ikiwemo kukosekana kwa wateja inafanya masoko hayo ya kisasa kutotumika ipasavyo kwani biashara inahitaji mzunguko wa wateja.

Mfanyabiashara mzoefu wa mazao ya jamii ya nafaka katika Soko la Tandale, Saidi Ngalawa licha ya kuishukuru serikali kwa uwekezaji mkubwa, anasema changamoto yao ni miundombinu ya barabara hali inayosababisha kutokuwapo kwa safari za magari yanayopita karibu na soko hilo.

“Kuna changamoto kuba hapa kwani hakuna wateja. …Ombi letu ni kupata ruti za daladala kutoka Mnazi-mmoja hadi Tandale kupitia Mburahati ili tupate wateja,” anasema mfanyabiashara mwingine, Shadia Issa.

Mfanyabiashara mwingine wa mbogamboga, Joyce Raphael anasema soko hilo litachangamka endapo kutakuwa na biashara ya jumla.

“Mfano wakati mahindi ya jumla yalivyokuwepo ilikuwa nafuu. Soko kama hili linatakiwa kuwa na vitu vingi vya jumla… Kuna miwa, lakini ni ya msimu; mahindi yarudishwe,” anasema Joyce.

Anaongeza: “Kabla soko halijajengwa, vitu vya jumla vilikuwepo. Mfano, machungwa yalikuwepo, mahindi, miwa; watu walikuwa wanatoka sehemu mbalimbali kuja kuchukua hapa sasa wale wakija kuchukua vitu vya jumla na hivi vitu vidogo vidogo lazima watachukua na sisi tunauza.”

Mwenykiti wa Soko la Tandale, Sultan Kiyumbo anasema soko hilo ni miongoni mwa masoko ya muda mrefu. Lilianizishwa mwaka 1972 kama soko la bidhaa za jumla. Ujenzi wa soko jipya ulianza 2019 na kuchukua kama miaka mitano mpaka Oktoba 2024 walihamia hapo.

“Maeneo mengi ya soko hayajatumika; kama kiongozi nina imani soko hili litajaa… Watu wengi walihama walipokuwa wanapisha ujenzi; waliobaki ndio waliohamia sasa na wengine wanafanya biashara maeneo yasiyo rasmi licha ya uwekezaji huu,” anaeleza.

Anasema soko hilo lina miundombinu yote kama maji, lifti, vyoo safi, ngazi za kawaida na ngazi kwa ajili ya watu wenye mahitaji maalumu, hivyo wanashukuru kwa kuwapo soko hilo la kisasa.

“Tunashauriana na halmashauri kubadilisha matumizi ya baadhi ya maeneo. Kama itawezekana, tunashauri pale juu tunaweza tukapatumia kwa kumbi za mikutano, sherehe, maeneo mengine mfano wale wa mahindi mabichi tunaendelea kushauri waje huku,” anasisitiza.

Kuhusuchangamoto za usafiri kutokana na kutokuwepo kwa daladala zinazopita maeneno hayo anasema: “Mtu akitaka kufungasha anaona shida ateremke Argentina au Kwa Tumbo saa tisa usiku; inakuwa shida. Tumewashauri watu wa mamlaka kurahisisha usafiri.”

“Tunatoa mwito kwa serikali wafanyabiashara waende katika maeneo rasmi. Kwa mfano, hapa tumezungwa kwa wauzaji wa mitumba waingie sokoni.

Anaongeza: “Wafanyabiashara wanapokaa sehemu moja wanawashawishi wateja wanawafuata. Kwa mfano, katika Soko la Mabibo; pale hakuna soko la kisasa na kuna matope mengi, lakini bado watu wanaenda kununua kwa sababu wafanyabishara wapo pamoja.”

Soko la Magomeni

Wafanyabiashara katika Soko la Magomeni wao wanalalamikia kukosekana kwa wateja licha ya eneo hilo kuwa na huduma zote yakiwemo maegesho na kuwa karibu na barabara.

Mfanyabiashara dawa za asili aliyejitambulisha kwa jina moja la Wiliam, anasema kufanya biashara hasa eneo la juu ya ghorofa ni vigumu kupata wateja kwa kuwa wananchi wengi hawana utamaduni wa kupanda maghorofa.

“Kuna siku inapita hauuzi kabisa. Miundombinu ni mizuri, lakini biashara ndio zimezorota hakuna hata watu wanaofika; hawapandi huku juu kwani pembeni ya soko pia watu wana maduka sisi wa ndani ni ngumu kupata wateja.”

“Soko la jumla hapa halipo kama lingekuwepo watu wangekuwa wanakuja kufuata bidhaa,” anasema.

Mfanyabiashara wa vinywaji maarufu, Mama Chuchuchu anasema: “Unaona hapa watu wanasinzia; tazama kama soko lingechangamka hakuna muuzaji angepata muda wa kusinzia.”

“Kama wangerudisha hoja ya kuwepo kwa soko la jumla, soko lingechangamka na mapato yangekuwepo mengi kuliko maelezo.”

Mfanyabiashara wa mbogamboga, Adelphina Martin anasema hali ya biashara imekuwa mbaya.

Wanaomba serikali itengeneze mazingira ya mwamko wa wateja ikiwa ni pamoja na kuwapo masoko ya jumla.

Anasema: “Hapa sokoni tunavumilia kwa sababu tumezoea ingawa kuna siku siuzi kabisa na kizimba Sh 500 natoa; meza imejaa mboga.”

“Hapa nawaza mambo kibao nyumbani watoto hawajala; watutafutie masoko ya jumla maana huko juu fremu ziko wazi wanaweza kubadilisha matumizi wakafanya ofisi ili mtu akitoka anakuja hapa kununua mboga.”

Mjumbe wa Kitengo cha Mbogamboga, Mariam Kimea anaeleza umuhimu wa soko la jumla kuongeza wateja sokoni na pia, umuhimu wa wafanyabiashara walio nje ya soko kuangaliwa upya.

Mfanyabiashara wa viungo, Nasra Selemani anasema biashara imedorora kwani anaweza kuuza tenga moja la nyanya hata kwa wikinzima kutokana na uhaba wa wateja. Anasisitiza uwepo wa biashara za jumla.

Mfanyabiashara mwingine mbogamboga na viungo aliyeko nje ya soko, anaeleza kwa namna hali ilivyokuwa ngumu ndani ya soko, waliamua kutoka nje huku akisema hata nje ya soko hakuna wateja wa kuridhisha.

“Askari walikuwa wanakuja kufukuza watu, nje lakini wakiondoka watu wanarudi kwenye maeneo ya nje kwa kuwa ghorofani biashara ni ngumu zaidi; afadhali kidogo nje ya soko.”

Mwenyekiti wa Soko la Magomeni, Daudi Dole anasema miongoni mwa sababu za biasahara kuzorota katika soko hilo ni pamoja na wakazi wengi wa Magomeni kuhama.

“Tulikuwa tunategemea watu wa Kiyungi; wote wamekwenda Mabwepande na baadaye Magomeni Kota wote wakaondoka na waliorudi hawanunui hapa ni wale wanaonunua mahitaji ya wiki, lakini wale wa kila siku hawapo.

“Nyumba nyingi Magomeni zimenunuliwa na matajiri; wanakaa watu wachache na wananunua vitu vya kuweka kwenye friji hadi watu wametoka nje ya soko kwa sababu ya ugumu wa kupata wateja,” anasisitiza.

Aidha, anashauri serikali kubadili matumizi baadhi ya maeneo na kuweka ofisi za serikali na binafsi hasa maeneno ya juu.

Anasema alikuwa anasimamia wafanyabiashara 925, lakini sasa ni 650 wengi wamekata tamaa wameondoka maeneo hayo.

Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo wa soko, wakati soko linajengwa walikubaliana kupokea wafanyabiashara 1,200 na ushuri wa Sh 500 kwa kizimba kimoja.

SOKO LA BWAWANI

Kutokana na ukosefu wa wateja katika Soko la Bwawani, serikali imeamua kubadili matumizi yake na kumpa mwekezaji ambaye sasa anafanya uboreshaji wa kufanya soko hilo kuwa maalumu kwa ajili ya mapambo.

Meneja Soko Bwawani, Nakazaeli Asumwisi anasema upungufu wa wateja ulisababisha wafanyabiashara kuhama katika soko hilo lililokuwa na vizimba 80 na fremu.

“Mazingira yalichangia hakuna barabara ambayo watu wengi wanapita na wakazi wengi wa hapa ni wale wanaonunua vitu vya muda mrefu; hapa karibu kuna Soko la Mwanyamala na wateja tayari walishazoea kule hivyo huku wakakosa wateja.”

Anasema soko hilo litakuwa la kwanza kwa vifaa vya mapambo nchini hivyo anatarajia wengi watapata maeneo na wateja kwani bidhaa za jumla zitaletwa hapo kutoka China.

Anabainisha kuwa, kuna fremu zaidi ya 70 kwa ajili ya biashara na wapambanji ni wengi.

Miongoni mwa wafanyabiashara wanaopanga kufanya biashara katika eneo hilo ni Mshereheshaji na Mpambaji (MC), Greace Meena. Anafafanua kuwa, wafanyabiashara wakikaa pamoja ‘watateka’ soko la hapo.

“Natarajia kuteka soko la ushereheshaji kwa sababu pia natumia mitandao na nina wateja wangu wanaonitafuta kupitia ushereheshaji,: anasema.

Anaongeza: “Naomba serikali katika hili Soko la Tanzania Weeding Plaza tunaomba magari ya daladala yapite hapa maana itasaidia watu kuzidi kujua eneo hili maana pia ni rahisi kwa watu kushukia karibu.

NAFASI YA MANISPAA

Katika masoko hayo, hali iliyopo inaonesha jitihada kubwa zinahitaji kwa halmashauri kuweka mikakati kwani hata baada ya kuanzisha masoko hayo bado usimamizi ni mbovu.

Hata hivyo masoko hayo yaliyojengwa kisasa bado usimamizi na uendeshaji wake umekuwa ukisuasua hivyo kusababisha halmashauri kuendesha kwa hasara.

Msimamizi wa Masoko Manispaa ya Kinondon, Goodluck Kabage anakiri kuwepo kwa changamoto lukuki zinazokabili masoko hayo kutokana na kuzorota kwa hali ya biashara.

“Ukianzisha kitu kipya changamoto huwa hazikosekani; ni kweli Soko la Bwawani tuliingiza wafanyabiashara na maeneo yote yalikuwa yamejaa vizimba 154 na fermu 31, lakini isivyo bahati utendaji kazi kibiashara haukuwa mzuri ikilingalisha na eneo lilivyo; masoko mengi yanazunguka hilo eneo.”

Anaongeza: “Kwa mazingira yale, walikuwa wanagawana wateja hivyo ni wachache na masoko ni mengine.”

Anasema ili Manispaa ya Kinondoni ihakikishe thamani ya fedha iliyowekwa inaonekana, iliamua kubadilisha matumizi kupitia taratibu za kisheria na kupangisha soko hilo kwa wawekezaji kwa kodi ya Sh milioni 50 kwa mwaka.

Kwa Soko la Magomeni anasema, wanaendelea kutatua changamoto zilizopo yakiwemo matumizikwani katika eneo la chini kuna wafanyabiashara wa mbogamboga, matunda na bidhaa zinapatikana.

Ghorofa ya kwanza ni kwa ajili ya huduma za nyama, samaki, mamalishe na mafundi nguo.

“Eneo la ghorofa ya pili kuna maduka ya bidhaa tofauti tofauti; ghorofa ya tatu ni sehemu ya ukumbi; kuna mwekezaji amelipia ukumbi na shughuli mbalimbali zinafanyika,” anasema.

Changamoto nyingine aliyoainisha ni wananchi kutokuwa na utamaduni wa kupanda juu katika masoko yenye maghorofa na hiyo imejitokeza katika masoko hayo kwani anasema wananchi wengi wamezoea masoko ya chini

“Kuna baadhi ya bidhaa zilipangiwa ghorofa ya kwanza, lakini watu hawakuitikia walifika pale na wakashuka chini na kulalamikia kuwa upande wa magohorofa wateja hawapendelei kupanda. Hizo ni miongoni mwa changamoto zilizojitokeza,” anasisitiza.

Kuhusu bidhaa za jumla katika soko hilo, anasema hilo ni suala la wafanyabiashara kuanzisha aina hizo za bidhaa na halmashauri iko tayari kupokea hilo na kusimamia utekelezaji wake kwani miundombinu yote inayohitajika ipo yakiwemo maegesho.

“Biashara za jumla zinaletwa na watu wa soko husika mfano, Soko la Tegeta Nyuki wanaouza vitu vya jumla ni wafanyabiashara waliotoka katika soko husika.”

“Tulishirikiana nao tukaunda kitengo na manispaa iliwapa gari waende sehemu nyingi wajifunze wenzao wanafanya nini?”

Kuhusu fremu zilizoonekeana zimefungwa, anasema nyingine zinafunguliwa kwa nyakati tofauti na pia ufanyaji biashara umebadilika; watu wanafanya biashara kwa njia ya mtandao kwa hiyo wateja wanaweza wasije sehemu bidhaa zinapopatikana.

Anabainisha kuwa Soko la Magomeni lina vizimba 343 na fremu 161 na ukumbi mmoja.

Kuna wafanyabiashara 789 na mapato kwa mwezi ni Sh milioni 6 huku kukiwa na mpishano kati ya idadi ya vizimba,fremu na idadi ya wafanyabiashara.

Anasisitiza kuwa, vizimba vyote vinatumika kwa kudai kuwa japo zinaonekana ziko wazi, ni za wafanyabiashara waliotoka nje ya soko na wanalipa kodi kama kawaida.

“Ufafanuzi wake ni kwamba wafanyabiashara waliopata changamoto walishuka chini; unaweza kuenda pale ukakuta vizimba viko wazi, lakini mapato tunapata kwani wafanyabiashara wamehamia chini wengine pambeni mwa soko na hapo mapato tunakusanya… vizimba vina watu.”

Anaongeza “Kwa vibanda vilivyo nje ya soko ni suala linalohitaji umaki;ni sana kwa sababu hawa watu walikuwa ndani wanatupa sana uchafu hapo kuendelea kuwang’ang’aniza kukaa ndani ni changamoto kubwa kuna mivutano lakini baada ya kushuka wanajitolea kulipa mapato,tunatafakari tuone namna gani tunawawekea mazingira rafiki yatakayoendena na biashara zao.

Aidha, anasema wanaangalia namna ya kupata wawekezaji watakaokuwa na mchango katika mapato kwa kutengeneza vizimba vilivyopo kama fremu kwa ajili ya ofisi za binafsi na za umma.

Kwa upande wa Tandale anasema changamoto zinafanana na zile za Magomeni hivyo wanaangalia njia za utatuzi ikiwemo kubadilisha matumizi ya maeneo kwa kujenga fremu eneo la vizimba na kujenga ukumbi kwa ajili ya sherehe na mikutano.

“Tandale ina wafanyabiashara 155 katika vizimba 425 vinavyotumika ni 155 tulianza makusanyo Septemba 2024 na mapato yake ni Sh milioni 120 kwa kipindi cha mwaka mmoja sasa,” anasema.

Goodluck anakanusha madai ya soko hilo kutofikika kirahisi huku akisema wameomba ruti za magari katika eneo hilo huku wakisumbiri kuanza kwa ruti hizo.

Anasema uratibu wa kupendezesha jiji ni mpango endelevu usio na kikomo kwani wanapokewa Wamachinga wapya kila siku.

“Tunajadili namna ya kudhibiti biashara zisizo katika maeneo rasmi na pia wateja wanaoenda kununua kama tukitengeneza sheria ndogo kwamba kununua bidhaa maeneo yasiyo rasmi utakuwa umevuja sheria itasaidia wajasiriamali wasiuze maeneo yasiyo rasmi,” anaeleza.

WACHUMI

Mtaalamu wa Masuala ya Biashara na Uchumi, Profesa Haji Sembojo anasema mpango wa serikali kuwa na masoko ya kisasa ni nzuri kwa kuwa wanataka kuwa na biashara rasmi ya watu wanaotambulika na bidhaa zinazouzwa ziwe zinazofahamika na zimesajiwa.

Anasema uelewa mdogo kwamba biashara si shughuli za kijiweni ni mfumo wa maisha bado ni changamoto kubwa hivyo mabadiliko yatachukua muda na kusisitiza serikali kupanga mfumo mzima wa utawala wa masoko.

“Kuona wengine wako nje wao wanaona ni sawa, lakini serikali inaweza kuhakikisha wote wapo ndani,” anasema.

Akitolea mfano ya Serikali ya Zanzibar, anasema inahakikisha biashara zinaundiwa sheria na taasisi zinazohusika na zinazosimamia maeneo ya biashara na upangaji wa mifumo ya biashara.

Kuhusu walaji, anasema zipo kasoro kwamba hawajajua namna nzuri ya kufanya ununuzi hata barabarani.

“Pamoja na mji kukua, vitu kama biashara vinatakiwa kuwekewa mfumo maalumu kama masoko ya jumla. Soko la Tandale ni sehemu ya watu wa Tandale na pia, maeneo mengine ni kwa watu ambao ni rahisi kufikia hivyo huduma za usafiri rahisi ni muhimu,” anasisitiza.

Mchambuzi mwingine wa Masuala ya Uchumi, Oscar Mkude anaeleza kuwa ni muhimu kutambua asili ya matumizi ya soko na namna ya ununuzi ya watanzania wengi masoko yao ni pembeni mwa barabara na wanaoenda masokoni kununua kwa jumla ni wachache.

“Watanzania wengi hawapendi kwenda sehemu kama hizo ni wavivu hata kupanda ngazi wanaona usumbufu kwenda juu hivyo wananunua chini au pembeni mwa barabara kwa urahisi hivyo wanahitaji kupata elimu na udhibiti.

Profesa Sembojo anasema: “Kwa upande wa mazao ya jumla, hilo pia ni muhimu. Kwa mfano, Soko la Ndizi la Mababo watu wengi kutoka maeneno mbalimbali wanaenda kununua pale na kwenda kuuza katika maeneo mengine; mtu akifika pale akaona kuna nyanya, karoti, hoho na vingine atanunua pia.”

Anashauri kujengwa masoko yanayoendana na watumiaji na pia, watu wapewe elimu kuhusu namna ya kutumia masoko katika ununuzi.

“Wafuatilie wajue kwanini watu wanapenda kununua vitu barabarani maana watumiaji wengi wanapenda urahisi, hivyo waangalie watumiaji wanataka nini na wajenge kwa kuangalia watumiaji,” anasema.

Anasema ni muhimu mamlaka kufanya utafiti kabla hawajajenga kadiri ya mahitaji ya watu kwani wakati mwingine wanataka soko la kawaida rahisi kuingia na kutoka.

“Wanunuzi wengi wanapenda masoko yaliyopo pembezoni mwa barabara; mahali ambapo kuna daladala zinapita au kituo cha mabasi,”anasema .

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *