
Katika taarifa iliyotolewa siku ya Alhamisi, Septemba 4, Volker Türk, Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Kibinadamu, ametoa wito kwa mamlaka mjini Bamako kuchukua “hatua madhubuti na za haraka kufuta sheria zenye matatizo” zilizopitishwa hivi karibuni nchini humo.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Kutolewa kwa mamlaka ya urais inayoweza kuongezwa bila uchaguzi kwa mkuu wa utawala wa kijeshi, kufutwa kwa vyama na mashirika ya kisiasa, na kuongezeka kwa idadi ya watu waliokamatwa kwa kutoa maoni yao tu: miaka mitano baada ya mapinduzi ya kijeshi dhidi ya serikali ya Rais Ibrahim Boubacar Keïta nchini Mali, Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Kibinadamu, Volker Türk ana wasiwasi kuhusu hali ya haki za binadamu katika nchi hiyo, “katika hali ya kuongezeka kurudi nyuma kwa demokrasia.” Kwa kuzingatia hili, Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Kibinadamu “anahimiza” mamlaka huko Bamako “kuchukua hatua madhubuti na za haraka za kufuta sheria zenye matatizo” zilizopitishwa katika miezi ya hivi karibuni, katika taarifa iliyochapishwa siku ya Alhamisi, Septemba 4.
“Tunasubiri hatua”
“Haya ni mabadiliko ambayo yamefunga mlango wa uchaguzi wowote wa kidemokrasia nchini Mali katika siku za usoni,” amesema Thameen Al-Kheetan, msemaji wa Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Kibinadamu, aliyewasiliana na RFI. “Huu ni ukiukaji wa haki ya kila raia kushiriki katika masuala ya umma nchini Mali, kupiga kura, na kuchaguliwa katika chaguzi halisi za mara kwa mara,” amebainisha, akiongeza na kubaini pia kwamba “ni muhimu kuchukua hatua za kuwaachilia mara moja na bila masharti wale wote wanaozuiliwa kiholela” nchini humo.
Wakati Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa pia anasikitishwa na ukiukwaji unaofanywa na makundi yenye silaha na wanajeshi wa Mali wanaoungwa mkono na wanajeshi wa Urusi kutoka “Africa Corps” dhidi ya raia na kutaka haki itendeke, “hata hivyo kuna nia iliyoonyeshwa ya kuendelea kufanya kazi na [taasisi yetu] kuboresha hali ya haki za binadamu nchini Mali,” anasema Thameen Al-Kheetan, ambaye anaongeza: “Lakini tunasubiri hatua.”