KAMANDA wa Polisi Mkoa wa Geita, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), Safia Jongo, ametoa wito kwa wazazi na walezi nchini kuhakikisha wanatekeleza wajibu wao ipasavyo katika malezi ya watoto ili kuzuia mmomonyoko wa maadili unaoweza kusababisha uvunjifu wa amani.
Akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Sozibuye, wilayani Geita, alipokuwa akiambatana na Mkuu wa Mkoa kukagua mradi wa shule ya msingi, Kamanda Jongo alisema jukumu la kulinda amani ya nchi linaanza katika ngazi ya familia. Kauli hiyo imekuja siku chache baada ya kutokea maandamano na vurugu zilizojitokeza kufuatia uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 29, 2025, ambazo zilisababisha uvunjifu wa amani katika maeneo kadhaa nchini.
“Serikali ya Awamu ya Sita inafanya kazi kubwa ya kuboresha miundombinu ya elimu ili kuwezesha watoto kupata maarifa na ujuzi wa maendeleo. Hivyo ni wajibu wa wazazi kuunga mkono juhudi hizo kwa kulea watoto katika misingi ya maadili,” alisema Jongo.
Aliongeza kuwa baadhi ya vijana wanaojihusisha na vitendo vya uvunjifu wa amani ni matokeo ya wazazi kushindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo katika malezi. “Mtoto anapopata elimu na malezi mema, tunapunguza vibaka mitaani. Lakini mtoto asiyeelimika na kukosa malezi, anakuwa tatizo kwa jamii. Kuandamana ni haki, lakini kuharibu mali za serikali ni uvunjifu wa amani,” alisisitiza.
Kamanda Jongo alionya tabia ya baadhi ya wazazi kuacha jukumu la malezi mikononi mwa walimu pekee, akisema hali hiyo inachangia ongezeko la vitendo vya uhalifu miongoni mwa vijana. SOMA: Polisi yaanika athari vurugu uchaguzi, yasaka wanane
Ametaka wazazi na jamii kwa ujumla kushirikiana kulinda rasilimali za nchi, hususan miundombinu ya elimu, akisisitiza kuwa uwepo wa amani ni msingi wa maendeleo endelevu ya taifa. “Miundombinu ya elimu ni hazina ya taifa. Wazazi tuwasaidie watoto wetu kuelewa uzalendo na thamani ya nchi yao,” alihitimisha Kamanda Jongo.
