RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, anatarajiwa kutangaza Baraza jipya la Mawaziri kesho, Novemba 13, 2025, katika hafla fupi itakayofanyika Ikulu Zanzibar.
Taarifa iliyotolewa na Kitengo cha Mawasiliano, Ikulu Zanzibar, imesema hafla hiyo itahudhuriwa na Wahariri pamoja na Waandishi wa Habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari, ambapo Rais Dk. Mwinyi atalitangaza kwa mara ya kwanza Baraza hilo pamoja na wizara zake.
Aidha, Dk. Mwinyi anatarajiwa kueleza dira kuu ya uongozi wa baraza jipya, itakayolenga katika utekelezaji wa vipaumbele vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), ikiwemo kuimarisha Uchumi wa Buluu, Uwekezaji, Huduma za Jamii, Miundombinu na Maendeleo Jumuishi kwa wananchi.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Baraza la Mawaziri wateule litakula kiapo cha uaminifu na uwajibikaji Jumamosi, Novemba 15, 2025, katika viwanja vya Ikulu Zanzibar. SOMA: Rais Mwinyi atangaza mwelekeo mpya SMZ
