DK. MWIGULU Lameck Nchemba ni miongoni mwa viongozi wa kisasa wa Tanzania wanaotambulika kwa umahiri katika taaluma ya uchumi na uongozi wa umma. Alizaliwa Januari 7, 1975 katika kijiji cha Makunda, wilayani Iramba, mkoani Singida.
Kutokea katika mazingira ya kawaida ya kijijini, alionesha mapema uwezo mkubwa wa kitaaluma na kiu ya mafanikio, hali iliyomuwezesha kupanda ngazi katika elimu, taaluma na siasa za kitaifa. Safari yake ya elimu ilianza katika Shule ya Msingi Makunda kabla ya kuendelea na elimu ya sekondari katika Shule ya Iboru na baadaye Shule ya Sekondari ya Mazengo.
Mwaka 2001 alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na mwaka 2004 akahitimu Shahada ya Kwanza ya Uchumi. Ufanisi wake chuoni ulimpa nafasi ya kuendelea na Shahada ya Uzamili ya Uchumi mwaka 2006 katika chuo hicho hicho.
Dk. Nchemba hakusita kujiongezea ujuzi zaidi. Miaka ya 2012 hadi 2018 alikamilisha Shahada ya Uzamivu (PhD) ya Uchumi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, jambo lililoimarisha uwezo wake wa kuchambua sera za kiuchumi na masuala ya maendeleo ya taifa.

Baada ya masomo, alianza kazi katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kama mchumi. Katika kipindi hicho, alipata uzoefu mkubwa katika masuala ya sera za fedha, uchambuzi wa uchumi na usimamizi wa mifumo ya kifedha. SOMA: Mwigulu amsifu Samia kutimiza maono ya Nyerere
Uzoefu huo ulijenga msingi imara wa uelewa wake kuhusu uchumi wa taifa, jambo lililomsaidia sana alipoingia katika siasa. Mwaka 2010, Dk. Nchemba aliingia rasmi katika ulingo wa siasa baada ya kuchaguliwa kuwa Mbunge wa Jimbo la Iramba Magharibi kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Umahiri wake wa kuchambua hoja na weledi wa kitaaluma ulimfanya kupata heshima kubwa bungeni na serikalini. Kutokana na uwezo huo, aliteuliwa kushika nyadhifa mbalimbali za uwaziri.
Amewahi kuwa Naibu Waziri wa Fedha, Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi (2015–2016), Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi (2016–2018), Waziri wa Katiba na Sheria (2020–2021) na tangu Machi 2021 amekuwa Waziri wa Fedha na Mipango.
Katika utendaji wake, Dk. Nchemba amejipambanua kwa nidhamu, uwajibikaji na matumizi bora ya rasilimali za umma. Ameendelea kusisitiza umuhimu wa kuongeza mapato ya ndani, kupunguza utegemezi wa misaada ya nje na kuhakikisha matumizi ya serikali yanakwenda sambamba na vipaumbele vya maendeleo ya taifa.
Kupitia Wizara ya Fedha na Mipango, ameweka mkazo katika kukuza uwazi wa matumizi ya fedha za umma, kuboresha ukusanyaji wa kodi na kusimamia utekelezaji wa miradi ya kimkakati inayolenga kuimarisha uchumi wa nchi.

Dk. Nchemba anajulikana kwa uongozi wa kitaalamu unaozingatia maamuzi ya msingi, ushauri wa wataalamu na ufuatiliaji makini wa utekelezaji wa sera za serikali. Mara kwa mara amekuwa akisisitiza umuhimu wa watumishi wa umma kuwajibika na kutumia fedha za walipa kodi kwa manufaa ya wananchi.
Licha ya changamoto za kimfumo na kiuchumi zinazolikabili taifa, ikiwamo usimamizi wa deni la taifa na mabadiliko ya kiuchumi duniani, Dk. Nchemba ameendelea kuaminiwa kutokana na umahiri wake na uwezo wa kuchanganua masuala kwa kina.
Elimu yake ya juu ya uchumi na uzoefu katika taasisi nyeti kama Benki Kuu ya Tanzania na wizara mbalimbali, zimemuwezesha kuwa kiongozi mwenye maono mapana katika kupanga na kutekeleza sera za maendeleo.
Kwa ujumla, Dk. Mwigulu Nchemba ni kiongozi mwenye misingi imara ya kitaaluma, uchambuzi wa kina na moyo wa uzalendo. Uongozi wake unaakisi dhamira ya kujenga Tanzania yenye uchumi imara, usawa wa kijamii na maendeleo endelevu kwa wananchi wote.