DODOMA: MBUNGE wa Isimani, William Lukuvi amesema Rais Samia Suluhu Hassan hakukosea kumteua Dk Mwigulu Nchemba awe Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Akiunga hoja ya serikali ya kuliomba Bunge lithibitishe uteuzi wa Dk Mwigulu kuwa Waziri Mkuu, Lukuvi alisema Rais Samia hakukosea kumteua kutokana na uwezo wake. “Namshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwawezesha Watanzania kufanya uchaguzi Oktoba 29,” alisema.
Pia, alimshukuru kwa kutekeleza kazi ya kikatiba ya kuleta jina Dk Mwigulu Nchemba bungeni ili lithibitishwe kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Alisema pamoja na sifa nyingine, Dk Mwigulu kwa muda mrefu amekuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM na Mjumbe wa Sekretarieti ya CCM na Naibu Katibu Mkuu.
“Hivyo, niwakumbushe wabunge wenzangu wa CCM, Rais Samia hakukosea. Kwani, pamoja na nyadhifa alizoshika na hajaingia kwenye siasa, Dk Mwigulu alikuwa anafanya kazi Benki Kuu ya Tanzania (BoT). Kama mnavyojua, Benki Kuu hawachukui watu wa hovyohovyo, bali wanachukua wenye uwezo.
“Mafaniko makubwa yaliyopatikana nchini chini ya uongozi wa Rais Samia na ambayo yamesaidia sisi wabunge kushinda kwenye maeneo yetu, yeye (Dk Mwigulu) ndio mkusanyaji ushuru. Tumthibitishe ili tumpe nguvu ya kuanza kazi.”
