Kishindo cha MwiguluKishindo cha Mwigulu

DODOMA:WAZIRI Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba amezielekeza hospitali zote nchini kuhakikisha wajawazito wanaofika hospitalini kuhudumiwa kwanza na hatua za kiutawala zifuatwe baadaye ili kuokoa maisha ya mama na mtoto.

Pia, aliagiza Wizara ya Afya, Bohari ya Dawa (MSD) na hospitali zote nchini ziweke vipaumbele vya kuwa na dawa muhimu kulingana na mahitaji. Dk Mwigulu aliyasema hayo jana alipofanya ziara ya kushitukiza katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma na kusema kwake ilikuwa ni ibada ya kutembelea wagonjwa.

Alisema haipendezi mjamzito kufika hospitali akiwa ana changamoto au hana changamoto kukaa mapokezi kusubiri kujiandikisha.

“Hivyo, naziagiza hospitali zote nchini, mjamzito ambaye ameshafika hospitalini awe na changamoto au hana changamoto, asisubiri kujiandikisha, apatiwe huduma kwanza, maana hawezi kutoroka na mafai li yamkute kitandani, asisubirishwe mapokezi,” alisema.

Vilevile, aliagiza hospitali zote nchini zihakikishe zinakuwa na vifaa vya usafi binafsi vya dharura, zikiwemo ndoo na beseni katika wodi za wazazi ili ziwasaidie wanawake wasiokuwa na vifaa hivyo na kusisitiza kuwa vifaa hivyo visiwe sababu ya kuchelewesha matibabu kwa wajawazito.

Pia, Dk Mwigulu aliielekeza Wizara ya Afya, MSD na hospitali kuweka vipaumbele vya kununua dawa kulingana na mahitaji na kusisitiza kuwa haipendezi kuzifanya hospitali kuwa vituo vya kuandikisha dawa na watu wakanunue katika maduka binafsi.

“Haipendezi mwananchi kufika hospitali na kupatiwa vipimo vyote, kisha anaambiwa dawa akanunue kwingine. Kama duka binafsi linaweza kupata dawa hizo, inawezekanaje hospitali za serikali hapati? Naagiza hospitali zote ziwe na dawa,” alisema.

Dk Mwigulu alisema amefarijika kuona wagonjwa na watu waliopelekwa kupata huduma katika hospitali hiyo wametoa mrejesho wa kuwa wamepokelewa na kuhudumiwa vizuri. Aidha, Dk Mwigulu alitumia fursa hiyo kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa alioufanya katika uboreshaji wa huduma za afya nchini.

“Nimewauliza wananchi ambao wana wagonjwa, wamekiri kupokelewa na wamepata huduma nzuri, hili limenifariji sana. Nitumie fursa hii kumpongeza rais kwa mafanikio haya. Viongozi wa hospitali chukueni maelekezo kwa watumishi wote, kuanzia mapokezi mpaka kwenye huduma ya mwisho, hatutegemei kitu tofauti na taaluma zenu,” alisema.

Pia, aliagiza hospitali zote nchini zizingatie maelekezo ya kutumia mifumo sahihi ya malipo katika taratibu za kutoa huduma ili kuwezesha serikali kuendelea kuhudumia wananchi. Dk Mwigulu alitoa agizo hilo kutokana na kuwepo kwa hospitali ambazo baadhi ya huduma wanapokea malipo kwa njia ya mtandao, nyingine malipo yanapokelewa kwa njia zisizo rasmi.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wagonjwa na wananchi wanaoguza ndugu zao walimpongeza Rais Samia kwa kuhakikisha wananchi wanapatiwa huduma bora za afya.

“Tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwa tunapatiwa huduma nzuri kama tupo hospitali za private (binafsi),” alisema mkazi wa Makulu jijini Dodoma ambaye amelazwa katika wodi ya wazazi, Dinna Enock. Aidha, Dk Mwigulu aliwataka wananchi kuwafichua watumishi ambao wanakiuka maadili ya utumishi wao kwa kutoa taarifa na kusisitiza kuwa, atawashukia kama mwewe.

“Hawezi mama yetu (Rais Samia) anakosa usingizi anahangaika kwa ajili ya Watanzania, watu wengine huku ambao wanatakiwa kufanikisha furaha ya Watanzania wanasababisha karaha, ni jambo ambalo halitakubalika na halitavumilika,” alisema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *