Bil 140/- kujenga barabara za IlalaBil 140/- kujenga barabara za Ilala

MKUU wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo amewaomba wananchi waendelee kuiunga mkono serikali kwa kuwa imetoa fedha nyingi za ujenzi wa barabara katika Jiji la Dar es Salaam hususani Wilaya ya Ilala.Mpogolo alisema hayo wakati wa ukaguzi wa miradi inayotekelezwa kupitia Mradi wa Maendeleo ya Jiji la Dar es Salaam, Awamu ya Pili (DMDP 2).

Amesema serikali imetoa takribani Sh bilioni 140 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya barabara katika wilaya hiyo pekee. “Natumia nafasi hii kumshukuru sana Rais Samia Suluhu Hassan ambaye ameleta fedha nyingi sana katika Wilaya yetu ya Ilala.

Daraja hili peke yake linagharimu zaidi ya Shilingi bilioni saba,” alisema Mpogolo wakati akikagua ujenzi wa Daraja la Majumba Sita-Segerea. Amesema Sh 138,237,462,371.37 zimetengwa kupitia DMDP 2 kujenga barabara zenye urefu wa zaidi ya kilometa 146.06 katika mikataba mitano inayoendelea kupunguza msongamano na kurahisisha shughuli za kiuchumi na kijamii.

Miradi inayotekelezwa inajumuisha ujenzi wa barabara za katikati ya jiji zenye zaidi ya kilometa 15 na barabara za Banana – Kitunda – Kivule Msongola na Kivule – Majohe Njia Nne. Pia, kuna ujenzi wa barabara za Migombani – Kiwalani, Banana – Kitunda, Baracuda – Chang’ombe – Majichumvi, barabara na Daraja la Majumba Sita – Segerea na Barabara ya Tabata – Maweni – Kisiwani.

Wakandarasi wanaotekeleza miradi hiyo ni pamoja na Jiangxi Geo Engineering Corp Ltd na Han Zhenliangni ndio Meneja Mradi na Mkandarasi wa Kivule wakati Wang Qingyong ni Meneja Mradi wa Segerea – Majumba Sita. SOMA: CCM yaja na mpango kuboresha barabara Moro

Amesema Daraja la Segerea – Majumba Sita ambalo ni muhimu kwa sababu linaunganisha Kata za Kiwalani na Segerea na muhimu kwa shughuli za kiuchumi na mahusiano ya kijamii linagharimu zaidi ya Sh bilioni saba na litakuwa na urefu wa zaidi ya meta 80 na ujenzi upo katika hatua za kuweka nguzo.

Kati ya nguzo 54 zinazotarajiwa kujengwa, tayari wameshafikisha nguzo 27, mkandarasi Jiangxi Geo Engineering Corp Ltd. Aliyewakilishwa na Wang amesema wanatarajia kukamilisha kazi zote za uwekaji nguzo mwishoni mwa mwezi huu ili kuanza ujenzi wa msingi wa daraja kabla ya msimu wa mvua kuanza.

Amesema utekelezaji wa mradi kwa ujumla umefikia asilimia tano na kukamilika kwa daraja hilo kutapunguza mzunguko mrefu ambao wananchi hulazimika kuufanya wakati mto unapojaa maji, hivyo kuokoa muda na kupunguza uchovu. “Daraja hili ni muhimu sana kwa watu wa Jimbo la Segerea, kiunganishi cha Kata ya Kiwalani na Segerea. Ni daraja ambalo lina umuhimu mkubwa kwa shughuli za kiuchumi,” alisisitiza Mpogolo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *