AMANI ni tunu adhimu ambayo kila taifa duniani hutamani kuipata na kuidumisha. Tanzania imekuwa kisiwa cha amani, hili ni jambo la kuendelea kujivunia sana kama Watanzania. Pamoja na tunu hii tuliobarikiwa nayo, tuna wajibu mkubwa kila Mtanzania kila kuhakikisha kuwa amani hii inaendelea kudumu kama nguzo kuu ya maendeleo yetu ya taifa.
Tunaamini katika misingi ya utaifa wetu, waasisi wa taifa wakiongozwa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere walisisitiza umuhimu wa umoja, upendo na mshikamano. Kwa nini walisisitiza ni kwa sababu waliamini kwamba bila amani, hakuna maendeleo, demokrasia, wala ustawi wa kijamii unaoweza kupatikana.
Ni wazi kwamba amani ndio chachu ya uwekezaji, elimu bora, huduma bora za afya na ustawi wa wananchi wote. Hata hivyo katika dunia ya sasa yenye changamoto za kiuchumi, mitandao ya kijamii na siasa za ushindani, amani yetu inaweza kutetereka endapo hatutakuwa waangalifu. SOMA: Samia ahimiza kuomba amani, ustahimilivu
Tuziepuke na kuziogopa sana kauli za uchochezi, misimamo mikali ya kisiasa na mgawanyiko wa kijamii kwani ni miongoni mwa mambo yanayoweza kuharibu misingi tuliyojenga kwa miaka mingi. Hivyo ni wajibu wa kila raia wa Tanzania kulinda na kuendelea kuitetea amani kwa matendo, maneno na fikra sahihi. Imani yetu huu ni wakati sasa wa kuwekeza zaidi katika elimu ya uraia, maadili na uzalendo.
Vijana waelimishwe kuhusu umuhimu wa amani kama urithi wa taifa. Viongozi wa kisiasa, kidini na kijamii wanapaswa kuwa mstari wa mbele kuhubiri umoja badala ya migawanyiko, vile vile wadau wengine vikiwemo vyombo vya habari vina jukumu kubwa la kuelimisha umma, si kueneza chuki au taarifa za upotoshaji.
Kuna usemi: ‘Umoja ni nguvu na Utengano ni udhaifu’, hivyo kwa pamoja tukiidumisha amani, Tanzania itaendelea kuwa mfano wa kuigwa barani Afrika na duniani kama taifa lenye utulivu, upendo na maendeleo endelevu. Watanzania tukumbuke tu amani ni nguzo ya maendeleo, tuilinde, tuiheshimu na tuiendeleze ili tuweze kutimiza mipango ya kulifanya taifa hili kupiga kasi zaidi katika maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kisiasa. Nasi hatutachoka kuihubiri amani kwa sababu ndio msingi wa utaifa wetu kama Watanzania.
